Inatisha! Njemba mmoja, Shadra
Maninje ‘Idd’, anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kuwaua watu wawili
na kujeruhi wengine wanne kwa kuwachoma visu sehemu tofauti za miili yao
akiwemo mtoto wa kike, Fatuma Hamis mwenye umri wa miaka miwili.
Wakizungumza na Wikienda lililofika eneo la tukio, kila shuhuda alikuwa na lake la kusema kutokana na mshangao walioupata.
“Hatujui nini kilimpata Idd kwani
alionekana amelewa na alipokuwa anakutana na mtu anamchomachoma visu.
Alimchoma Miraji Kondoa kisu cha kifuani na kufariki dunia.
“Pia inasemekana kuna mwanachuo wa NIT wa kike alimchoma kisu na yeye alifariki dunia.
“Mbali na hao alimchoma kisu
mfanyabiashara aliyefahamika kwa jina la Jackson Mushi ‘Rasta’ sehemu ya
tumboni na utumbo kuonekana. Baadaye wasamaria walimpeleka Hospitali ya
Mwananyamala.
“Baada ya kufanya matukio hayo, watu
walianza kumkimbiza huku wakiwa wameshika mawe. Alipoona hivyo alikimbia
na kupotelea uchochoroni lakini cha ajabu alipofika huko nako alimchoma
kisu mwanafunzi wa NIT,” alisema mmoja wa mashuhuda huyo akiungwa mkono
na mwingine:
“Mbali na huyo kuna mama mwingine ambaye
hajafahamika naye alichomwa kisu cha tumboni na kutokezea mgongoni na
inasemekana hali yake ni mbaya sana.”
Katika tukio hilo, wanahabari wetu
walizungumza na mmoja wa majeruhi ambaye ni mwanafunzi wa NIT, Maiko
Erasto (26) ambapo alisimulia:
“Nilikuwa ndani na mwenzangu, ghafla
tulisikia kishindo cha kitu kuanguka nje, nikatoka ili kufahamu
kilichotokea, nilipofungua mlango nikamuona jamaa ambaye sikuwa
namfahamu, akanyanyua kisu kunichoma kichwani nikakwepa lakini
kikanipata begani.
“Baada ya kuona vile, mwenzangu
alinivuta chumbani na kuufunga mlango, kumbe pale nje kulikuwa na mtoto
wa kike (Fatuma Hamis) ambaye naye alichomwa kisu shingoni na ameshonwa
nyuzi 8.”
Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa Jitegemee,
Kilema alikiri kutokea kwa tukio hilo la kusikitisha na kusema kuwa kuna
watu walipoteza maisha na wengine kujeruhiwa na mtuhumiwa huyo ambaye
alikamatwa na kufikishwa katika Kituo cha Polisi cha Urafiki jijini Dar.
Wakazi na wafanyabiashara wa
Mabibo jijini Dar es Salaam wakiwa wameizunguka ofisi ya soko la
Mabibo-Mwisho alimohifadhiwa mtu anayetuhumiwa kuua na kujeruhi watu
kadhaa katika soko hilo kabla polisi hawajafika.