Bunge jana lilielezwa kuwa msanii aliyebuni na kutengeneza nembo ya taifa ya Bibi na Bwana, Francis Ngosha ametelekezwa na taifa na anaishi maisha magumu.
Suala la msanii huyo liliibuka Bungeni mjini Dodoma leo, kutokana na mwongozo ulioombwa na Mbunge wa Temeke (CUF), Abdalah Mtolea, ambaye amesema msanii huyo hajanufaika na ubunifu wake huo.
“Kwa muda mrefu tumekuwa tukipiga kilele hapa tukidai haki miliki ya wasanii wetu ili kazi zao ziweze kuwanufaisha wao na familia zao,”amesema Mbunge huyo akiegeme kanuni ya 68(7) na 47(1).
“Kumekuwa na kilio na malalamiko makubwa ya Bwana Francis Ngosha ambaye ndiye aliyebuni ngao (nembo) ya taifa ambayo tunaitumia kwa kiasi kikubwa na tunajivunia ngao hii,”amesema.
“Lakini mtu huyu hajawahi kunufaika kwa kazi hii ya mikono yake anaishi pale Buruguni maisha ya ajabu maisha mabovu, afya yake ni mbaya na anashindwa hata kwenda kupata tiba,”amesisitiza.
“Anaishi kwa shida wakati ngao yake inaheshimika hata hapa kwenye jengo letu. Hivi kweli na sisi kama Bunge tunaingia kwenye dhambi hii ya kula jasho la mtu ambalo hajalipwa haki yake?”amehoji.
Akijibu muongozo huo, Mwenyekiti wa Bunge, Azzan Mussa Zungu, alisema kwa maoni yake haoni sababu ya shughuli za bunge kuahirishwa ili kujadili suala hilo bali Serikali ilitolee maelezo.
“Hili la kwako halina udharura litajibiwa na waziri wa nchi (Jenister Mhagama). Inawezekana Serikali ina majibu yake ama mmemsaidia lakini zile pesa zikaenda zikapigwa na watu pembeni,”amesema.
Mhagama ambaye ni Waziri wa Nchi ofisi ya Waziri mkuu anayeshughulikia Sera,Bunge,Kazi,Vijana, Ajira na Walemavu, alisema Serikali italichukua suala hilo kuona njia bora ya kulishughulikia.
“Serikali inampongeza sana msanii huyu kwa kuweza kufanikisha nchi yetu kuwa na nembo tunayojivunia wote. Sisi kama Serikali tunapaswa kuichukua,”amesema Mhagama na kuongeza;-.
“Tutakwenda kuangalia namna hoja hii itaweza kupewa uzito. Kwa ujumla naomba niseme msanii amefanya kazi kubwa sana na taifa letu limeendelea kutambulika kwa kutumia kazi hiyo,”amesema.