Tundu Lissu Amtumia Salamu Waziri Ummy Mwalimu...Adai Atamjibu Mwenyewe

Nafasi za Ajira Zilizotangazwa Leo Bonyeza Hapa
RAIS wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Tundu Lissu,  ameibuka na kusema, “vijembe vinavyorushwa na Ummy Mwalimu,” Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, “vitajibiwa na mimi mwenyewe,”

Akihutubia mkutano wa nusu mwaka wa mawakili nchini (AGM), kaka mkubwa wa Lissu, Alute Mughwai Lissu, ameeleza kuwa ameelekezwa na mdogo wake huyo, kutomjibu Ummy Mwalimu, badala yake kazi hiyo itafanywa na yeye mwenyewe.

Alute ambaye ni wakili wa kujitegemea anayefanya shughuli zake mkoani Arusha ameuambia mkutano huo, “nimeongea na Lissu leo saa nne asubuhi. Amenielekeza kuwa familia isijibu hoja za waziri Ummy Mwalimu.”

Amesema, “kazi hiyo itafanywa na yeye mwenyewe mara akataporejea nchini kutoka kwenye matibabu yake nje ya nchi. Ameahidi kuendeleza mapambano ya kudai haki bila kuchoka.”

Wakili Alute amesema, Lissu amemueleza kuwa “hatarudi nyuma katika harakati zake za kutetea haki na demokrasia nchini. Ameapa kupambana hadi tone lake la mwisho.”

Kwa mujibu wa Alute, afya ya Lissu inaendelea vizuri na anawashukuru madaktari wanaomtibu kwenye hospitali ya Nairobi alikolazwa. Amewataka wajumbe wa mkutano huo kuendelea kumuombea.

Alute alikuwa akitoa salamu kwa wajumbe wa mkutano mkuu wa TLS uliofanyika jana mjini Arusha.

Hii ni mara ya kwanza kwa Lissu kuzungumza kwa simu tokea aliposhambuliwa kwa risasi na wanaoitwa na serikali, “watu wasiofahamika,” ambako alimiminiwa rundo la risasi zilizolenga kuondoa maisha yake.

Wakati huohuo, akiongea na Azam TV, Alute Lissu amesema kwamba familia yake imemwandikia barua Mwanasheria Mkuu wa Serikali wakiomba uchunguzi wa tukio la kushambuliwa mdogo wake ufanywa na vyombo kutoka nje ya nchi, kwani katika mazingira ya sasa jeshi la polisi haliko tayari na haliko huru kufanya uchunguzi huo kwani hadi sasa hakuna mtu yeyote aliyekamatwa.

Kuhusiana na serikali kuitaka familia iandike barua ya kuomba matibabu kwa ajili ya Tundu Lissu, kaka yake huyo alisema mdogo wake huyo ambaye anatibiwa Nairobi amemwambia suala hilo atakuja kulizungumzia yeye akiwa ni mbunge mwenye haki zote za kupewa matibabu kama wabunge wengine.

Vyanzo: Mwanahalisi na Azam TV.
_________

 Nafasi za Ajira Zilizotangazwa Leo na Makampuni Bonyeza HAPA

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad