Albino Wanaangamia, Serikali Haina Habari


LEO tumechapisha katika ukurasa wa kwanza habari za kusikitisha kuhusu jinsi Watanzania wenzetu wenye ulemavu wa ngozi (Albino), wanavyoendelea kupoteza maisha kutokana na sehemu ya jamii yetu kukumbwa na imani potofu za kishirikina, kwamba viungo vya watu hao vinaleta utajiri mkubwa na wa haraka.  Ni imani hizo potofu ambazo zimeikumba jamii yetu tangu mwaka 2000 wakati nchi yetu kwa mara ya kwanza ilianza kushuhudia mauaji ya kinyama dhidi ya ndugu zetu hao.

Dunia ilishangazwa na jambo moja kubwa kuhusiana na hali hiyo. Kwamba ilikuwaje Tanzania iliyokuwa ikiheshimika duniani kama kisiwa cha amani, kimbilio la wanyonge na kinara wa kuheshimu haki za binadamu ilibadilika ghafla na kujihusisha na vitendo hivyo vya kinyama? Watanzania wengi waligubikwa na aibu isiyo kifani na walishindwa kuamini kuwa, hakika vitendo hivyo vilikuwa vikitokea ndani ya mipaka yetu.

Makundi yote katika jamii yaliibana Serikali ikomeshe unyama huo na kuliondolea taifa aibu hiyo. Bahati mbaya Serikali haikuonyesha dhamira ya kutokomeza uovu huo, bali ilibakia kutoa machozi ya mamba, huku mauaji ya ndugu zetu hao yakiendelea kuripotiwa katika sehemu nyingi nchini. Serikali na Bunge vilishindwa kuweka mkakati wa kupambana na watu waliokuwa wakifanya uovu huo, angalao kwa kutunga sheria kali dhidi yao na kuwatia mbaroni waganga wa kienyeji waliokuwa wakichochea vitendo hivyo.

Jambo la ajabu ni kwamba Serikali iliendelea kuikumbatia  sheria dhaifu ya mwaka 1928 ambayo haina meno. Kutokana na hali hiyo, mauaji hayo yamekuwa yakitokea sehemu nyingi nchini hadi hivi sasa, huku Serikali ikiwa haijui kinachoendelea. Hii imetokana na ukweli kwamba kesi nyingi zilizofunguliwa mahakamani dhidi ya wauaji wa watu hao zimekuwa zikisuasua kutokana na Serikali kutoona umuhimu wa kesi hizo kusikilizwa kwa hati ya dharura. Matokeo yake watuhumiwa wengi wa mauaji hayo bado wanachekelea.

Tumesema yote hayo kuonyesha udhaifu wa Serikali katika kusimamia na kuratibu vita dhidi ya mauaji ya Albino. Kama habari tuliyochapisha leo katika ukurasa wa kwanza inavyoonyesha, tumerudi nyuma kama taifa katika kukomesha unyama dhidi ya ndugu zetu hao. Mtafiti na mwanaharakati wa masuala ya Albino hapa nchini, Vicky Ntetema ambaye kwa muda mrefu amekuwa akisafiri nchi nzima kuripoti hali hiyo, ametoa ripoti inayothibitisha pasipo shaka kwamba watu hao bado wanawindwa kwa ajili ya viungo vyao.

Katika utafiti wake katika baadhi ya mikoa, ikiwamo Tabora na Rukwa, amebaini kwamba waathirika wa unyama huo sasa wamekatwa mikono ya kushoto. Hali hii anasema imeacha maswali mengi. Je, mizimu ya waganga wa kienyeji kama wao wanavyodai kuelekezwa na mizimu hiyo, safari hii imeamua waganga hao wapelekewe mikono ya kushoto? Mtafiti huyo anasema kuwa, huko nyuma waganga hao walikuwa wakitaka kupelekewa mikono ya kulia.

Mtafiti huyo amebaini kwamba mwezi huu, watu watatu wamekatwa viungo na mmoja wao kuuawa. Kwa muhtasari tu, anasema kwamba tangu mwaka 2000 yamefanyika mashambulizi 123 ambapo watu 72 walipoteza maisha. Kati ya watu 34 walionusurika, wengi wao walikatwa viungo au kuumizwa vibaya, huku makaburi 15 yakifukuliwa na viungo vya watu hao kuibwa. Ni majaribio manne tu ya kufukua makaburi ndiyo yaliyoshindwa.

Serikali inastahili lawama kwa kuendelea kuwapo kwa hali hiyo. Inakuwaje zaidi ya nusu ya waganga wa kienyeji bado hawajasajiliwa na Serikali? Inakuwaje wanaachwa waendeshe shughuli hizo kwa kuegemea uchawi na ushirikina?

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad