Azam Yaijaza Presha Yanga
0
February 22, 2013
KITENDO cha Benchi la Ufundi Yanga kwenda ‘kuishushu’ Azam ilipokuwa Uwanja wa Chamazi kucheza na JKT Ruvu, ni ishara kuwa mchezo wa vinara hao kwenye msimamo wa ligi kesho utakuwa mgumu na usiotabirika.
Azam sasa imefikisha pointi 33, sawa na Yanga inayoongoza ligi baada ya kuifunga JKT Ruvu mabao 4-0 katika mchezo wa katikati ya wiki hii.
Kocha Mkuu Yanga, Ernets Brants na msaidizi wake, Fredy Minziro walikacha mazoezi ya timu yao Bagamoyo na badala yake kwenda Chamazi kuipeleleza Azam. Makocha hao waliopatwa na wakati mgumu wa kuzomewa na mashabiki, walifika Chamazi dakika 5 kabla ya kuanza mchezo na kwenda kuketi jukwaani.
Wakiwa jukwaani, walionekana wakiteta huku pia wakiandika mambo kadhaa, ambayo huenda ilikuwa ni kuandaa mikakati ya ushindi kwenye mchezo wa kesho.
“Wana wasiwasi na Azam, hawajiamini,” alisema shabiki mmoja wa Azam aliyeketi karibu na makocha hao. Aliongeza: “Kwa jinsi Azam ilivyo kwa sasa, hakuna uwezekano wa Yanga kuifunga.”
Mara baada ya mchezo kumalizika, Kocha wa Azam, Stewart Hall alisema hana wasiwasi na mchezo dhidi ya Yanga, kwani kikosi chake kiko makini. “Kuna baadhi ya wachezaji hawakucheza katika mchezo wa leo kutokana na kuwa majeruhi lakini naamini kwa siku mbili hizi hali zao zitakuwa vizuri,” alisema Hall. Kocha Ernest aliiambia Mwananchi kuwa, Azam ni timu nzuri na wamejipanga kushusha jeshi la kweli ili kupata ushindi kwenye mchezo wao unaofuata.
“Nilikuwa Chamazi, nimeiona Azam ni timu nzuri na yenye uwezo mkubwa. Lakini sina shaka na wachezaji wangu, watacheza kwa nguvu zote,” alisema Brandts.
Kuhusu kambi ya timu yake Bagamoyo, Brandts alisema haikuwa maalumu kwa ajili ya mchezo dhidi ya Azam, ila kwa mechi zote za ligi.
“Mazingira ya kambi mazuri, wachezaji wanapata fursa ya kukaa pamoja na kushiriki mazoezi bila shida yoyote,” alisema. “Ninachoweza kusema, wachezaji wangu wote 26 wako salama, sina majeruhi. Nategemea wataonyesha mchezo wa ushindi kama tulivyofanya kwenye mechi zilizopita.”
Imeandikwa na Jessca Nangawe, Vicky Kimaro na Clara Alphonce.