Fifa Yaingilia Kati Uchaguzi wa TFF

SHIRIKISHO la Soka Duniani (Fifa) limeingilia kati uchaguzi mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania baada ya kupokea malalamiko ya baadhi ya wagombea pamoja na kuangalia upya katiba ya TFF kama ina makosa.
Katika barua ya Fifa iliyotumwa TFF na kusainiwa na Naibu Katibu Mkuu wa Fifa, Markus Kattner, imeitaka TFF kusimamisha uchaguzi kwa muda hadi wajumbe wake watakaokuja nchini katikati ya mwezi Machi kuangalia upungufu huo kabla ya kutangaza upya tarehe ya kufanyika kwa uchaguzi huo.
Akizungumza jijini jana Rais wa TFF,  Leodeger Tenga alisema wamepokea barua kutoka Fifa juu ya ujio wa wajumbe watakaochunguza malalamiko hayo ambayo yaliwasilishwa huko na baadhi ya wagombea wakipinga uamuzi uliotolewa na kamati inayosimamia uchaguzi huo chini ya Mwenyekiti wake Iddi Mtiginjola iliyowaondoa kwenye kinyang’anyiro hicho.
Tenga alisema yeye kama mtendaji mkuu wa TFF hatapenda kuona uchaguzi huo ukifanyika bila haki na badala yake atasimamia kikamilifu akishirikiana na Fifa katika kuweka sawa jambo hilo.
“Kwanza kabisa nawashukuru Fifa kwa kuitikia wito huu wa wapenda soka kwani hii imeonyesha wanatujali na kuthamini mpira wetu, naamini baada ya ujumbe huo kila mmoja ataridhika na majibu yatakayotolewa kwani ni vyema tukachelewa kufanya uchaguzi, lakini kila mmoja akawa na imani na viongozi watakaochaguliwa kwa kufuata haki,” alisema Tenga.
Aliongeza “Wapo baadhi wamepeleka malalamiko Fifa, sawa kwetu hiyo ni changamoto na tumeipokea kwa mikono miwili kwani walichosema Fifa watatuma ujumbe ambao utajumuisha wanasheria na wasuluhishi wa migogoro katika kuliweka hili wazi, naamini uamuzi wao ndiyo utatoa majibu katika kufanyika kwa uchaguzi,” alisema Tenga.
Alisema zipo hatua tatu za kuchukua endapo kutatokea malalamiko kwa wagombea ambazo ni kufanya marejeo, kukata rufaa au kupeleka kwenye mahakama ya soka CAS.
Kuhusu fursa ya kufanya marejeo kwenye Kamati ya Rufani ya Uchaguzi inayoongozwa na Idd Mtiginjola ambayo aliielezea Jumamosi, Rais Tenga alisema kwa vile hicho ndicho chombo cha mwisho nchini katika masuala ya uchaguzi alishauriwa kuwa kingeweza kufanya hivyo.
“Kwa vile hakuna chombo kingine, nikashauriwa kuwa kinaweza kufanya marejeo. Katika utaratibu wa kutoa haki, uamuzi ni lazima uwe wa wazi kwa kutoa sababu. Nilidhani hilo linawezekana, kwani Mahakama Kuu hufanya hivyo. Kwa hili uamuzi wa Mtiginjola ni sahihi,” alisema Rais Tenga.
Katika hatua nyingine, Tenga alikanusha kufanyika mkutano mkuu kwa siri kwa nia ya kubadilisha baadhi ya vipengele na kusisitiza walichofanya ni kupewa ridhaa na wanachama wao katika kuweka sawa baadhi ya vipengele ili viweze kutumika kwa usawa katika uchaguzi mkuu.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad