Kufaulu Mitihani Vizuri Sio ‘Kipaji Maalumu’
0
February 27, 2013
Kuna huu utaratibu uliozoeleka kwamba watoto wanaofaulu vizuri mitihani yao ya kuhitimu darasa la saba na kidato cha nne huchaguliwa kujiunga katika shule zinazoitwa “Shule za Watoto Wenye Vipaji Maalum”. Baadhi ya shule hizi ni Ilbouru, Mzumbe, Msalato, Tabora, Kibaha na Kilakala. Kila siku nimekuwa nikijiuliza: ni vipaji gani walivyo navyo hawa watoto wanaochaguliwa kujiunga na shule hizi? Hivi kumbe kufaulu mitihani vizuri ni “kipaji maalum”? Je, ni kweli kwamba hizi ni shule za watoto wenye “vipaji” maalum? Na ni vipaji gani hivyo?
Nijuavyo mimi kipaji maalum ni kama vile kipaji cha ufundi, kusakata mpira (soka), kutunga, kuimba au kucheza muziki; ushonaji, useremala, uashi, uchoraji, ubunifu wa mitindo ya mavazi, n.k. Nitajitahidi kueleza. Kwa mfano, kuna wachoraji ambao akikuangalia mara moja tu, anaweza kukuchora sura yako kama ulivyo bila kukosea. Hawa wana kipaji maalum cha kuchora. Sio kila mtu anayeweza kuchora kwa ufasaha hata kama akiigilizia kitu anachokichora. Ikiwa huwezi kufanya hivyo, basi ujue kwamba huna kipaji cha kuchora.
Katika nchi zilizoendelea, watoto wenye vipaji kama hivi hugunduliwa mapema na kutengewa shule maalum ambazo hutumika kuendeleza vipaji vyao. Wengi wa wanasoka wanaosifika ulimwenguni wana vipaji vya kucheza mpira. Vipaji vyao vilionekana tangu wangali wadogo na vikaendelezwa. Kufaulu vizuri masomo sio kuwa na kipaji maalum. Serikali imeshindwa kuibua au kugundua vipaji vya watoto na kuviendeleza, badala yake imekuwa ikiwahadaa wananchi kwamba kufaulu vizuri ndiyo kipaji maalum!
Kuna wagunduzi mbalimbali katika nchi hii ambao kama serikali ingekazana kuendeleza vipaji vyao tungeondokana, kwa kisasi fulani, na matumizi makubwa ya pesa katika kununua teknologia na kuajiri wataalamu kutoka nje. Katika miaka ya hivi karibuni, kuna mtanzania mmoja aligundua mashine ya kusaga nafaka ambayo hutumia nguvu za maji yanayotiririka. Mwingine aligundua teknologia ya kutengeneza ndege kwa kutumia vyuma chakavu na kufanikiwa kuirusha angani kwa dakika kadhaa. Na wa mwisho aligundua teknolojia ya kurusha matangazo ya redio. Endapo serikali yetu ingekuwa makini ingeviendeleza vipaji vya wagunduzi kama hawa na hatimaye tukaja kuwa na teknologia yetu sisi wenyewe ambayo baadaye tungeomba msaada kutoka nje tukaiboresha na kufikia teknologia kamili.
Uzoefu unaonesha kwamba wagunduzi wengi wa karne iliyopita hawakuwa na uwezo mkubwa sana darasani kama hawa vijana wetu “tunaowabatiza” kuwa “wenye vipaji maalum”. Mfano mzuri ni Bill Gates ambaye aligundua teknologia na matumizi ya kompyuta. Huyu mtu hakuwa mzuri sana darasani na inasemekana kwamba alikimbia shule (school dropout). Ila kwa kuwa serikali yake ilikiona na kukithamini kipaji chake, haikusita kukiendeleza. Hatimaye tumepata kompyuta, nyenzo ambayo imesaidia sana kurahisisha kazi za kila siku za mwanadamu.
Mpaka hapo nadhani tumeishaona tofauti kati ya kufaulu vizuri darasani na kipaji maalum. Hivyo basi, serikali iache kutupaka mafuta kwa mgongo wa chupa kwa kutuaminisha kwamba hapa Tanzania tunazo shule za watoto wenye vipaji maalum! Jibu ni kwamba hakuna shule hata moja ya aina hiyo katika nchi hii; badala yake tunapumbazwa bure kwa kuaminishwa kitu ambacho hakipo. Tija ya hizo shule (wanazosoma watoto waliofanya vizuri kimasomo) kwa maendeleo ya taifa, kama ipo, ni kidogo sana. Hazitoshi kuifanya serikali itoke kifua mbele kwa kutenga shule za namna hiyo. Wananchi tuweni makini na baadhi ya kauli za serikali. Akili za kuambiwa, tuchanganye na za kwetu!