Matokeo kidato cha nne ‘feki’
• Mkurugenzi Green Acres afichua siri nzito
WAKATI mjadala wa matokeo mabaya ya kidato cha nne ukiendelea kulitikisa taifa, kashfa mpya ya matokeo hayo imeibuliwa.
Kashfa
hiyo mpya imeibuliwa na Mkurugenzi wa Shule ya Green Acres, Julian
Bujugo, kwamba matokeo ya baadhi ya shule nchini ikiwamo yake
yamechakachuliwa.
Akizungumza
na gazeti hili jana, Bujugo alisema kuwa baadhi ya wanafunzi kwenye
shule yake hawakufanya mitihani ya kidato cha nne, lakini matokeo
yanaonesha wamefaulu kwa kupata alama za juu.
Alitaja
mfano wa mwanafunzi, Humphrey Sanga, mwenye namba 01197/148, ambaye
hakufanya mitihani hiyo lakini matokeo yanaonesha amefaulu kwa kupata
alama nzuri.
“Huyu mwanafunzi
tulimsimamisha na hakufanya mitihani, lakini matokeo yake yanaonekana
amepata hivi; Civics D, Historia D, Jiografia C, Kiswahili D, English
C, Physics D, Chemistry C, Biology C, Basic Mathematics D, ambapo
amepata daraja la tatu pointi 24,” alisema Bujugo.
Alimtaja mwanafunzi mwingine, Martin Rushaigwa, namba 01197/0173, ambaye alifanya masomo ya ‘Arts’.
Alisema
matokeo ya mwanafunzi huyo yanaonesha kuwa ameongezewa alama za masomo
ya biashara ya Bookeeping na Commerce, ambayo hakuyafanya kabisa.
Alimtaja
mwanafunzi mwingine aliyefanya mtihani huo lakini matokeo yake
yanaonesha amewekewa ‘absent’ na mwanafunzi mwingine, Mbazi Volta,
hakufanya mitihani lakini amepewa alama za ufaulu.
“Matokeo hayo yananipa wasiwasi kwamba yanaweza kuwa yamechakachuliwa,” alisema Bujugo.
Mkurugenzi
huyo anaiomba Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kurudia kusahihisha
mitihani hiyo ili kuondoa ukungu ulioligubika taifa kwa sasa kuhusu
matokeo ya kidato cha nne.
“Naomba
usahihishaji urudiwe, maana huu ni ubabaishaji mkubwa…matokeo hayo
yamewaathiri watoto kisaikolojia na sijui watakwenda wapi?,” alihoji.
Alisisitiza
kuwa usahihishaji urudiwe kwani katika shule hiyo wanafunzi wenye
uwezo mkubwa tangu walipoanza kidato cha kwanza ndio waliofanya vibaya
wakati waliokuwa wakifanya vibaya, wameibuka na alama za juu.
Mkurugenzi
huyo alisema wazazi wa watoto hao wanatarajiwa kukutana mwishoni mwa
wiki hii kujadiliana kuhusu matokeo hayo na hatua za kuchukua.
Akitolea
ufafanuzi suala hilo, Msemaji wa Baraza la Taifa la Mitihani (NECTA),
John Nchimbi, alisema si kweli kuwa matokeo hayo yamechakachuliwa bali
ni matokeo halisi ya shule hiyo.
Alisema
iwapo mkurugenzi wa shule hiyo ana shaka na matokeo hayo, alitakiwa
kufika katika ofisi za baraza hilo ili apatiwe taarifa sahihi kabla ya
kutoa taarifa katika vyombo vya habari.
“Mi
nimeangalia hayo majina, naona yapo sawa na hata huyo mwanafunzi
ambaye anasemekana hakufanya mitihani na akapewa alama…napenda kusema
kuwa alama alizopewa si zake na hata katika orodha yetu anaonekana kuwa
hakufanya mitihani,” alisema.
Katika
hatua nyingine, Waziri wa wizara hiyo, Dk. Shukuru Kawambwa na
wenzake, wamekuwa bubu kueleza endapo wako tayari kujiuzulu au la.
Tanzania
Daima ilifika wizarani hapo jana kutaka kuonana na Waziri Kawambwa ili
atoe msimamo wake, mwandishi alijibiwa kuwa waziri huyo alikuwa
kikaoni na asingeweza kutoka.
Hata waziri alipopigiwa simu pamoja na kutumiwa ujumbe mfupi wa maneno, hakupokea wala kujibu ujumbe huo.
Kwa upande wake, katibu mkuu wa wizara hiyo naye hakuwa tayari kuzungumzia suala hilo kwa madai kuwa alikuwa kikaoni.
Naye
Naibu Waziri, Philipo Mulugo, alipotafutwa kupitia simu yake ya
mkononi kueleza msimamo wake, simu yake iliita bila kupokewa na hata
hakuwa tayari kujibu meseji ya ujumbe mfupi.
hii ni number yangu co ya huyo
ReplyDeleteBY James
ndio lazima tusikubali
ReplyDeleteKwa mwendo huu tutafika kweli?
ReplyDelete