Polisi waanza kuwafuatilia waliomtukana Spika

POLISI mkoani Dar es Salaam wametangaza kuwafuatilia, kuwasaka na kuwachukulia hatua wote waliotuma ujumbe wa matusi ama kupiga simu ya vitisho kwa Spika wa Bunge, Anne Makinda.

Viongozi wa Chadema walifanya mkutano wao mwishoni mwa wiki kwenye Viwanja vya Mwembe Yanga, Temeke, jijini Dar es Salaam na kutoa namba za Spika wa Bunge ili mashabiki wamshinikize ajiuzulu.
Pia viongozi hao walitoa namba za simu za Naibu Spika, Job Ndugai ili naye ashinikizwe ang’oke katika nafasi yake kwa madai ya kukandamiza upinzani bungeni.

Chadema walidai kuwa Makinda na Ndugai wamekuwa wakipindisha kanuni wakati wa kuliongoza Bunge. Pia walidai kuandaa taarifa ya kutokuwa na imani na maspika hao, ripoti ambayo wataiwasilisha kwenye Bunge lijalo.

Wakati Polisi wakitangaza hayo, juzi Ofisi ya Bunge kupitia kwa katibu wake, Thomas Kashilillah ilisema itawachukulia hatua kali wale wote waliotumia lugha chafu kwa ujumbe mfupi ama kupiga moja kwa moja kwa Spika na Naibu wake.

Hatua hiyo ya polisi inachukuliwa baada ya Makinda kudai kuwa ametumiwa ujumbe mfupi zaidi ya 400 na kupigiwa simu zisizopungua 200, zinazomkashifu na nyingine zikiwa ni za vitisho dhidi yake.

Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Ahmed Msangi alisema Polisi watafanya uchunguzi kuwabaini wote waliohusika kufanya hivyo na hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao ili iwe fundisho kwa wengine.

Msangi alisema kuwa taarifa hizo wamezipata jana na walijipanga kuhakikisha wahusika wote wanatiwa mbaroni.

“Polisi tumeanza kuwafuatilia waliomtukana Spika na lazima tuwakamate kwani kitendo hiki ni kinyume cha sheria,” alisema Msangi.
Akizungumza na gazeti hili ofisini kwake jana, Kaimu Ofisa Mawasiliano wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Semu Mwakyanjala alisema suala la vitisho kwa mtu yeyoye linahusu hasa Jeshi la Polisi na kwamba wao ndio wanaopaswa kuchukua hatua zaidi za kisheria.

Wanachama wa CCM Mkoa wa Iringa, wamelaani vikali kitendo cha baadhi ya wafuasi wa Chadema kutuma ujumbe mfupi wa simu za mkononi kumkashifu Makinda huku baadhi yao wakipendekeza chama hicho kifutwe kwa kukosa ustaarabu.

Katibu wa Baraza la Wazee wa CCM Wilaya ya Iringa, Said Mdota alisema kitendo alichofanyiwa Spika Makinda si cha kiungwana na hakikubaliki na wapenda amani wote. Mdota alipendekeza wahusika wote wasakwe na wachukuliwe hatua kali za kisheria.

Naye Mwenyekiti wa Jumuiya wa Wanawake Mkoa wa Iringa, UWT, Zainab Mwamwindi alisema jumuiya hiyo inatarajia kukutana kesho pamoja na agenda nyingine itajadili suala hilo na kulitolea tamko.

“Sisi kama wanawake na Spika ni mwanamke, suala hili limetudhalilisha sana na katika hili tunalikemea kwa nguvu zote na Februari 14, tunatarajia kufanya kikao cha Kamati ya Utendaji tutalijadili na kulitolea tamko,” alisema.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad