TAIFA Stars, leo itashuka dimbani kuwakabili Cameroon, katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki utakaopigwa kuanzia saa 11:00 jioni kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kocha Mkuu wa Stars, Kim Poulsen, amesema wamejiandaa vizuri kwa ajili ya mchezo huo na kwamba wachezaji wote wapo fiti isipokuwa Said Nassor ‘Chollo’ aliyeumia mazoezini.
“Tupo tayari kwa ajili ya mchezo huo, tunajua Cameroon ni timu nzuri na ina mastaa wengi wenye vipaji.
“Nawataka wachezaji wawe makini na watengeneze nafasi za kufunga. Naamini tutafanya vizuri,” alisema Kim ambaye alisisitiza anaweza kuwatumia Mbwana Samatta na Mrisho Ngassa kama mawinga ili kuongeza mashambulizi.
Kwa upande wake nahodha wa Stars, Juma Kaseja, amesema wanaamini watafanya vizuri kutokana na maandalizi waliyoyafanya.
“Mchezo utakuwa mgumu, wao watakuwa 11 na sisi 11, kwa hiyo tuna uwezo wa kushinda, tunaomba sapoti ya Watanzania,” alisema Kaseja.
Naye Kocha wa Cameroon, Akono Seanambaye, amesema: “Tutapata jaribio jipya la kuchuana na Watanzania, tunaiheshimu sana timu hiyo.”
Wachezaji wengine wa Cameroon wakiongozwa na nahodha wao, Samuel Eto’o, walitarajiwa kutua nchini jana usiku kwa ajili ya mchezo huo.
Taifa Stars Kuwachinja Kina Samuel Eto’o Leo
0
February 06, 2013
Tags