TFF wakesha airport kumsubiri Eto’o



PAMOJA na mashabiki wa soka Tanzania kutarajiwa kupata burudani ya kutosha kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya Cameroon leo, viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wamekesha kwa siku tatu kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere.
Timu ya Cameroon imekuwa ikitua nchini kwa mafungu kuanzia Jumapili usiku hadi jana mchana saa nane ambapo alitua kiungo Benoit Assou-Ekotto.
Mshambuliaji hatari wa Cameroon, Samuel Eto’o  mpaka jana alasiri alikuwa hajatua hapa nchini na kiongozi mmoja wa juu wa TFF pamoja na dereva walikuwa wakihaha kwa siku tatu uwanjani hapo.
Filamu ilianza Jumapili jioni baada ya viongozi hao kuambiwa kuwa kuna baadhi ya wachezaji pamoja na viongozi wa benchi la ufundi watatua, lakini walipokwenda walirudi makwao usiku wa manane kutokana na kila mara kubadilishiwa shirika la ndege.
“Wamekuwa wakielezwa kuwa Eto’o pamoja na wachezaji wengine wanakuja saa tatu asubuhi lakini wakifika pale wanakaa mpaka saa tano usiku bila kuambulia chochote.
“Wamekuwa wakifika hapa na kupata baadhi ya wachezaji, lakini wakati mwingine wanakuja saa sita mchana wanakaa mpaka usiku mnene ndiyo wanaondoka.
“Lakini huu ujio wa Eto’o umewasumbua sana, kila wakati wanaambiwa anakuja na ndege fulani wanakimbia kuja hapa, lakini hawaambulii chochote, jana (juzi) wametoka hapa usiku mnene, leo tazama hadi sasa bado hawajamuona.
“Waliambiwa anakuja asubuhi, wamefika hapa mapema sana na sasa ni alasiri wanaondoka na bado hawajaambulia kitu, nasikia wameambiwa waje hapa usiku saa tano,” kilisema chanzo.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad