Utalii wa Ngono Waingia Nchini


Baadhi ya vivutio hivi ni Mlima Kilimanjaro, mbuga za wanyama, majengo ya kale, mapango na nyumba za kihistoria.
KATIKA hali ya kawaida, tumezoea kuona watalii kutoka mataifa mbalimbali duniani wakija nchini kuangalia vivutio vya utalii vilivyopo.
Baadhi ya vivutio hivi ni Mlima Kilimanjaro, mbuga za wanyama, majengo ya kale, mapango na nyumba za kihistoria.

Hata hivyo, kumeibuka aina mpya ya utalii, unaojulikana kama utalii wa ngono, ambao unashamiri kwa kasi ukihusisha zaidi watalii wanawake wanaofuata wanaume wa Kitanzania hasa vijana.

Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi Jumapili, unaonyesha kuwa utalii huo unaongezeka kwa kasi hasa katika maeneo yenye vivutio vingi vya utalii ikiwamo Arusha, Kilimanjaro na Zanzibar.

Imebainika kuwa katika utalii huu, wanawake hasa watu wazima walio na umri kati ya miaka 60 hadi 80 kutoka nchi mbalimbali, wamekuwa wakiingia nchini kwa lengo la kutafuta vijana wa kiume wa kustarehe nao.

Uchunguzi huo unaonyesha kuwa wanawake ambao hawana vigezo vya uzuri vinavyopendwa na wanaume huko kwao, ikiwamo wembamba na urefu, husafiri kuja Tanzania kutafuta mwanamume atakayestarehe naye kingono.

Hali hiyo inawakumba zaidi wanawake wanene, ambao kwa Ulaya hukosa wapenzi, hivyo kulazimika kusafiri kuja Afrika Tanzania ikiwamo kutafuta mwenza wa kustarehe nao.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa, utalii huu umeshamiri nchini, ambapo vijana wa Kitanzania wanaufahamu na kukiri kuwa umewanufaisha na baadhi yao kuwasaidia kupata tiketi za kwenda kuishi Ulaya.

Katika Visiwa vya Zanzibar utalii huo unafanyika zaidi katika fukwe za Nungwi, Kiwengwa, Paje, Kendwa, Jambiani na maeneo mengine yaliyopo pembezoni mwa bahari.

Katika fukwe hizo vijana maalumu kwa kazi hiyo, wana kauli mbiu yao inayosema:“apewe mpaka apagawe, atoe tiketi.”

Kwa kauli mbiu hiyo vijana hao wanamaanisha kuwa, kwa kila mwanamke watakayekutana naye, watatumia kila mbinu ili kumfurahisha hadi awasafirishe au kwenda naye Ulaya.

Abdulla Ali Haji (Sio jina halisi) ni miongoni wa vijana wanaojihusisha na aina hiyo ya utalii, akiishi visiwani humo ambapo anaeleza kuwa shughuli yake kubwa ni kuzunguka katika fukwe mbalimbali akiwinda wanawake wa kizungu wanaotaka kustarehe.
“ Kweli kuna wanawake wengi wa kizungu wanakuja huku kwa ajili hiyo tu, hasa wazee. Kwa kuwa tunatafuta pesa na tiketi za kwenda Ulaya, hatujali mwanamke huyo ana umbo gani wala umri,” anasema Abdulla.
Anaongeza: “Wazungu wengi wanakuja kututafuta kwa sababu sisi tuna nguvu za kutosha, nasi tunajituma kwa sababu tunataka kuondoka katika maisha haya.”

Alibainisha kuwa wengi wa watalii wa aina hiyo wanatokea katika nchi za Norway, Holland, Belgium, Sweden na Finland.

Naye Hamis Mgodo anabainisha kwamba utalii huo umekuwa visiwani Zanzibar na kwamba wao wanaweza kumtambua mwanamke anayetafuta starehe hiyo kwa kumtazama tu.

“Ni biashara inayojulikana kabisa, mwanamke aliyekuja kwa ajili hii utamjua tu. Sisi humfuata au yeye hukueleza shida yake, kinachofuata ni juhudi zako binafsi kwani hawa wanakuja kutafuta starehe, akiipata vizuri, hawezi kukubali kuiacha Bongo,” alisema Mgodo.

Alidokeza kuwa vijana wengi wanaishi kwa kutegemea utalii huo kwa kuwa wanawake hao wazee huwalipa vizuri, hivyo kupata pesa nyingi tofauti na kazi nyingine ambazo kwa kibarua huweza kupata kati ya Sh3000 hadi 5000 kwa siku.

“Kwa siku anaweza ‘kukutoa’ na Dola 300 hivi, kama akifurahi dau linaweza kupanda mpaka mwenyewe ukashangaa. Lakini anaweza kukufurahisha zaidi pia pale anapoondoka kurudi kwao, kwani anaweza kukuachia kila kitu kama ‘laptop’, simu, kamera na pesa nyingi,” alisema Mgodo.

Kijana mwingine anayejihusisha na biashara hiyo anaeleza kuwa yeye ni wa dini nyingine, lakini alibadili jina na kuitwa Dave Bryson baada ya kupata mwanamke wa kizungu.

“Dini siyo kikwazo kwa ‘ma beach boy’ wengi kwa kuwa wanachoangalia wao ni kusafiri tu iwapo nafasi itapatikana. Mimi nina rafiki zangu wengi, walikubali kubatizwa na kufunga ndoa kanisani ili mradi tu waondoke nchini,” anasema Bryson na kuongeza:

“Hakuna anayejali dini hapa, kila mtu anataka kusafiri, wako radhi wabatizwe hata na maji gani, lakini kama mwisho wa siku wataondoka hawalijali hilo.”

Jiji la Arusha

Katika jiji hilo pia kuna makundi ya vijana waliovutiwa na kujihusisha na utalii huo, huku wanaojihusisha na biashara ya vitu vya utalii vikiwamo mapambo, vinyago na michoro ya aina mbalimbali wakitajwa zaidi.


Uchunguzi unaonyesha kuwa baadhi ya watalii hao wa ngono, huingia nchini kwa lengo la kufanya shughuli za kijamii za kujitolea, lakini hulowea kwa utalii wa ngono, hata kuhamia kwenye makazi ya vijana hao.
Vijana wa jamii ya Kimasai pia wametajwa kuathirika zaidi na utalii wa ngono, ambapo wengi wao wamekuwa wakionekana katika mitaa ya Jiji la Arusha wakiranda na kinamama wazee wa kizungu.

Makutano ya watalii wa aina hiyo yamekuwa katika kumbi mbili kubwa za burudani jijini humo, moja ikiwa katikati ya jiji na nyingine nje ya jiji ambapo, watalii wamekuwa wakifurika zaidi nyakati za jioni.

Hata hivyo, baadhi ya Watanzania ambao wamejihusisha na utalii huo, wamefaidika kwa kuanzishiwa kampuni za utalii na wengine kusafirishwa nje ya nchi, hali ambayo imekuwa ikivutia vijana wengi kujihusisha zaidi wakiwamo pia madereva wa magari ya kubeba watalii.

Wakizungumza na Mwananchi Jumapili katika mahojiano maalumu, baadhi ya walionufaika na utalii huo wa ngono, wameeleza kuwa mara nyingi wateja wao, wamekuwa ni kina mama wazee ambao ni wastaafu.

“Mimi nipo na mama mmoja kutoka Uingereza kwa miaka mitatu sasa. Kila mwaka anakuja kunitembelea, anajua kuwa nina mke, lakini hana shida na amekuwa akimpenda mke wangu,”alisema kijana mmoja wa jamii ya Kimasai.

Kijana huyo mkazi wa Wilaya ya Simanjiro, alisema kuwa mwanamke huyo, pia amekuwa akimtumia fedha za matumizi mara kwa mara, hali ambayo inaongeza ubora wa maisha yake na kumfanya aendelee kuwa naye.

“Mimi kama ninapata fedha nina shida gani? Yule mama amenieleza kabisa yeye anataka starehe na mimi. Ni mtu mzima ambaye hana shida kwao kwani wanalipwa pensheni,” alisema kijana huyo.

Kijana mwingine alifafanua kuwa, alikutana na mtalii wake, katika Ukumbi wa Masai Camp mjini Arusha miaka mitatu iliyopita na baada ya kupendana naye amekuwa akija nchini kila mwaka.

“Mimi nina mpenzi wangu mzungu, ndiye ambaye amenijengea nyumba. Ana familia yake Ujerumani na mume wake alifariki miaka mingi,” alisema kijana huyo, ambaye alikuwa katika kundi moja maarufu ya burudani mjini Arusha.

Baadhi ya vijana wa Kitanzania, ambao wamelowea katika utalii wa ngono, wamepata fursa ya kuhamia katika nchi wanazotoka wanawake hao na kuanza maisha mapya.

Katika Jiji la Arusha kuna kampuni kadhaa za utalii ambazo zimeanzishwa na watalii wa ngono, ambao walifikia nchini kutalii na baadaye kufanikiwa kupata wapenzi wa kudumu.

Mmoja wa vijana, ambao hufanya kazi ya kutembeza wageni katika Mbuga za Serengeti, mkoani Mara, Sospeter Nyambi (sio jina lake halisi) ameliambia gazeti hili kuwa wanawake hao wenye umri wa kuanzia miaka 50-60 hufika nchini kwa ajili ya utalii, kubwa ikiwa ni kufanya ngono na vijana wenye umri wa kati ya miaka 20-25.
“Huwalipa vijana kuanzia Dola 600 hadi 1,000 wanapokuwa nao, wanaonaswa zaidi na mchezo huo ni wabeba mizigo ya wageni (Care Take),”anasema na kuongeza:

Mmoja wa watembeza wageni kutoka kampuni moja iliyoko jijini Arusha alisema, wageni wanao kuja nchini kwa kazi hiyo hukaa kwa siku moja hadi wiki moja na wakati mwingine hawahami kupata hoteli.

“Alitaja vivutio vingine wanavyopewa vijana wa Kitanzania zaidi ya Dola za Kimarekani ni safari za Zanzibar, Nairobi, Mombasa na nyingine zilizopo nje ya Bara la Afrika.

Alibainisha kuwa wapo ambao baada ya kunogewa na penzi la vijana, hubaki nchini kwa muda wakijidai wameolewa kwa kisingizio cha kuanzisha kampuni za kutembeza wageni hata kwa gari moja.

“Mimi nimepoteza rafiki yangu kwa maana ngono wanazofanya na hawa akinamama ni nzembe na wengi wanakuja huku wakiwa ni wagonjwa. Kama hakutakuwa na mfumo wa ufuatiliaji vijana wengi watakufa kwa Ukimwi,” alisema kijana huyo.

Alipoulizwa yeye kama ameishashiriki mchezo huo alisema kuwa mwaka 1997 alikutana na mama mmoja akiwa na nia hiyo, lakini hawakufanikiwa kufanya ngono.

Alibainisha kuwa akina mama hao hufanya juu chini kuhakikisha wanazaa na vijana hao ili wabaki nchini kwa kuanzisha kampuni za kusafirisha wageni.

Kinachowavutia watalii kwa vijana

Kwa uzoefu wao vijana wengi wanasema, watalii hawa wanavutiwa na vijana ambao siyo watanashati, wanapenda yule anayeonekana mchafu.

Mwonekano wa vijana wa kimasai unawavutia wazungu wengi, hata wale ambao siyo kabila hilo kwa asili wamekuwa wakivalia hivyo ili kuweza kuwavutia.

Pia, uchunguzi umeonyesha kwamba wanawake wa kizungu wanapenda vijana wenye rasta, wakiamini kuwa siyo wahalifu.
Mkuu wa Kitengo cha Mahusiano wa Bodi ya Utalii nchini, Geofrey Tengeneza alipotakiwa kulitolea ufafanuzi suala hili alisema, ni geni kwake ingawa alikiri kufahamu aina hiyo ya utalii.
Tengeneza alisema anafahamu kuwa, aina hii ya utalii umeingia Afrika Mashariki isipokuwa kwa Tanzania hakuwa na taarifa zozote.

“Ninaufahamu utalii huu, wenzetu Afrika Mashariki hasa katika miji ya Mombasa na Nairobi si jambo geni, ila sikutegemea na kwetu unaweza kufika kutokana na mila na desturi zetu,” alisema na kuongeza.

“Sifahamu kama kwetu utalii wa aina hii upo wala sikuwahi kufikiria kama unaweza kuingia kwa kuwa vijana wetu wamelelewa katika maadili mazuri,” alisema Tengeneza.

Hata hivyo, Meneja Uhusiano wa Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa), Pascal Shelutete alisema kuwa bado shirika hilo haliutambui utalii wa ngono.Utalii wa ngono waingia nchini - Kitaifa - mwananchi.co.tz

Post a Comment

2 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Mimi nimeachana na boyfriend wangu kisa alipata mwanamke wa kizungu
    Haki vijana wa kitanzania wanakwisha hawa wanawake wanawamaliza

    ReplyDelete
  2. This is quick-witted. I've heard this kind of thing not too long ago though this is quite accurate. Kudos

    Feel free to surf to my web-site :: Author's
    external home page...

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad