Katika taarifa yake jana, Tendwa alisema kifungu namba 9(2)(c) cha sheria ya vyama vya kisiasa ya mwaka 1992 kikisomwa pamoja na kifungu 5 (b)(i) kama kilivyorekebishwa mwaka 2009 kinakataza vurugu, fujo, matumizi ya nguvu na uvunjifu wa amani wa aina yoyote na kuwa ni kosa la jinai linalopaswa kufanyiwa kazi na mamlaka.
Tendwa alisema matukio kama hayo yanatengeneza taswira mbaya ya siasa nchini na kushusha heshima na imani ya wananchi kwa vyama vya siasa.
Alisema ofisi ya msajili inachukua suala hili kwa kuvihusisha vyama husika ili ipate ukweli na undani wake na iweze kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa sheria.
Alisema,ofisi yake inavikumbusha na kuviasa vyama vya siasa kuheshimu sheria za nchi, sheria ya vyama vya siasa na maadili ya vyama vya siasa.
Viongozi na wafuasi wa vyama hivyo walipigana hadharani wakigombea uwanja wa kufanyia mikutano.
CHANZO: NIPASHE