Yanga na Azam Uwanjani Leo, Nani Atashinda?
0
February 23, 2013
YANGA na Azam zinacheza leo Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. Inawezekana ndio mechi tamu zaidi kishabiki na kiufundi tangu kuanza kwa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara.
Ni mechi ngumu ambayo kila timu inahitaji ushindi kumtimulia vumbi mwenzake kwenye mbio za kuwania ubingwa wa Bara ingawa Simba yenye pointi 31 ikiwa imenasa kwenye nafasi ya tatu inaombea angalau timu hizo zitoke sare kwani yoyote kati yao akishinda atafikisha pointi 39 ambazo kwa Simba si nzuri hata kidogo.
Azam na Yanga kila moja iko fiti na ina wachezaji wake wote muhimu ukiondoa baadhi waliosimamishwa wa Azam kama Erasto Nyoni, Aggrey Morris na Said Morad ambao walikuwa nguzo kwenye kikosi cha kwanza.
Yanga chini ya kocha Mdachi Ernest Brandts itaanza hivi; Ally Mustapha 'Barthez', Mbuyu Twite, Oscar Joshua, Kelvin Yondani, Nadir Cannavaro, Athuman Idd 'Chuji', Simon Msuva, Frank Domayo, Didier Kavumbagu, Jerry Tegete na Haruna Niyonzima.
Lakini Azam yenye pointi 36 kama Yanga kwa mujibu wa mazoezi ya wiki hii kwenye uwanja wa Chamanzi itaanzisha kikosi hiki; Mwadini Ally, Himid Mao, Malika Ndeule, David Mwantika, Joackins Atudo, Kipre Balou, Hamphrey Mieno, Salum Aboubakary, John Bocco, Kipre Tchetche, Abdi Kassim/Hamis Mcha.
Uwepo wa Domayo na Chuji kwenye kiungo cha Yanga utakuwa burudani ya aina yake ingawa Azam nayo ina Salum Abubakary ambaye atakuwa tegemeo kubwa katikati kwavile amekuwa kwenye fomu kipindi kirefu.
Mao, Ndeule na Mwantika wamekuwa tegemeo na ukuta mzuri wa Azam kwenye mechi za hivi karibuni kama walivyo Mbuyu, Yondani na Cannavaro wa Yanga ambayo ilipiga kambi ya muda mjini Bagamoyo.
Timu hizo mbili zimekuwa wapinzani wakubwa tangu msimu uliopita baada ya kutokea vurugu katika mchezo wao wa mzunguko wa pili uliosababisha wachezaji wa Yanga wakiongozwa ne beki wa kushoto Stephano Mwasyika kumpiga mwamuzi Israel Mkongo na kusababisha mechi hiyo kusimama kwa dakika kadhaa kabla ya baadaye amani kurejea uwanjani na mchezo kuendelea lakini hata hvyo Azam ilishida mabao 3-1.
Lakini Yanga wakaja kulipiza kisasi timu hizo zilipokutana tena msimu huu kwenye mzunguko wa kwanza wa ligi kwa ushindi wa mabao 2-0 yakifungwa na Hamis Kiiza na Didier Kavumbagu, hivyo mashabiki wanasubiri kujua nini kitatokea ndani ya dakika 90 leo Jumamosi.
Vita ya aina yake itakuwa upande wa washambuliaji kwani timu zote mbili zina washambuliaji wenye akili wanapofikia katika lango la timu pinzani.
Azam wakimtegemea Kipre Tchetche na John Bocco wakati Yanga watakuwa wakipeleka mashambulizi kupitia kwa Tegete na Kavumbagu huku Said Bahanuzi na Hamis Kiiza wakianzia benchi kuusoma mchezo.
Tegete aliiambia Mwanaspoti kuwa "Azam ni timu kubwa na ina wachezaji wazuri lakini kipigo kwao kiko pale pale," alisema Tegete kwa kifupi huku akisisitiza ataonyesha vitendo uwanjani.
Ingawa moyoni watataka kuona angalau sare, lakini ni wazi kwamba Simba watakuwa upande wa Azam ili iifunge na kuiondoa Yanga kileleni.
Kocha wa Yanga Ernest Brandts alisema; "Tutacheza mpira wa kasi kubwa kuhakikisha tunapata mabao ya mapema, kwani Azam ni moja ya timu nzuri na ndio maana ipo juu kwenye msimamo na lazima tuwe waangalifu."
Naye kocha wa Azam Stewart Hall alisema: "Kelele za mashabiki wao hazituzuwii kuwafunga Jumamosi, nimewaambia wachezaji wangu wanatakiwa kushusha presha na kucheza kwa uhuru wasisikilize kelele za nje kwani Yanga wanafungika hivyo mashabiki wetu waje kwa wingi uwanjani."
Yanga na Azam zote zina pointi 36, Azam ikiwa imecheza mechi 17 imeshinda 11, imetoa sare tatu na imepoteza michezo mitatu huku ikifunga mabao 31 na imefungwa mabao 14 wakati Yanga wamecheza michezo 16, wameshinda 11, wametoa sare mitatu, wamepoteza miwili, wamefunga magoli 33 na wamefungwa 12.