Kuzinduliwa kwa bodi mpya ya Shirika la Viwango Tanzania (TBS), mwanzoni mwa wiki kunaonekana kuanza kuleta matumaini kwamba huenda taasisi hiyo hatimaye ikafanya kazi zake kwa ufanisi na kupambana na tatizo la uingizaji nchini bidhaa feki.
Tunasema hivyo kwa kutilia maanani ukweli kuwa, tangu shirika hilo lianzishwe kwa sheria ya Bunge ya mwaka 1975, hakuna anayeweza kusema kwa hakika kwamba shirika hilo limefanya kazi kwa ufanisi na mafanikio na kufikia malengo yaliyowekwa.
Tatizo kubwa lililolisibu shirika hilo kwa miongo mingi ni kukosa uongozi wenye ubunifu, dira na mwelekeo kiasi cha wafanyakazi na viongozi kukumbatia utamaduni wa kufanya kazi kwa mazoea.
Tunaambiwa kwamba bodi mpya iliyozinduliwa juzi imeanza kazi kwa kishindo. Mara baada ya kuzinduliwa ilitangaza kumung’oa aliyekuwa akikaimu nafasi ya mkurugenzi mkuu na kutangaza hatua ya kuwasaili upya wakurugenzi wa vitengo vyote katika shirika hilo.
Kwa rungu alilopewa na Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Abdallah Kigoda wakati akiizindua bodi hiyo, Mwenyekiti wa bodi hiyo, Profesa Cuthbert Mhilu alimtangaza Joseph Masikitiko kukaimu nafasi ya Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo.
Hapana shaka hatua hiyo iliwashtua viongozi na wafanyakazi wa shirika hilo, ambalo kama tulivyosema hapo juu limekuwa likifanya kazi chini ya viwango, tena kwa kusuasua.
Ni shirika lililokumbatia vitendo vya rushwa na lililoshindwa kuwaleta wafanyakazi pamoja au kujiwekea malengo na kuhakikisha malengo hayo yanafikiwa. Uzembe huo umesababisha soko letu la ndani livamiwe na bidhaa feki kwa asilimia 30.
Hivyo, ni sahihi kabisa kwa bodi hiyo mpya kwanza kupitisha fagio la chuma katika shirika hilo, ili kuweza kuondoa uozo na kujipanga vizuri kukabiliana na changamoto nyingi ambazo menejimenti imeshindwa kuzitatua.
Changamoto hizo ni pamoja na kusimamia masuala ya ubora wa bidhaa zinazozalishwa na kuuzwa hapa nchini kutokana na kuibuka kwa viwanda bubu vinavyozalisha bidhaa feki.
Bodi hiyo itafanikiwa iwapo itashirikiana vyema na mamlaka nyingine, zikiwamo Baraza la Taifa la Kutetea Walaji na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA). Vinginevyo nchi yetu itageuzwa kuwa dampo la bidhaa duni.
Wakati tukisema hayo, ni matumaini yetu kwamba Serikali italiwezesha shirika hilo kuweka na kusimamia viwango vya bidhaa na huduma nchini, mbali na kuhakikisha kwamba shirika hilo linapata wafanyakazi wa kutosha, vifaa na maabara ya kisasa ili kudhibiti ubora wa bidhaa zinazozalishwa nchini na zinazotoka nje.
Kama saivi tanzania bidhaa feki zimekithiri kwa uwingi mbaka watu tunakua tunaogopa kununua vi2 mfano betri za magari,' oil ya engine za gari na spare zote za magari kwa ujumla....!!!
ReplyDelete