HUKU ikidaiwa kwamba ni wapenzi, mastaa wawili wa fani tofauti, mcheza filamu na mwanamuziki, Zuwena Mohammed ‘Shilole’ na msakata kabumbu wa klabu ya Simba, Mrisho Ngassa, Jumatano iliyopita walizua timbwili katika klabu ya usiku ya SunSiro iliyopo Ubungo jijini Dar.
Kwa mujibu wa chanzo chetu, Ngassa alifika katika klabu hiyo saa saba za usiku kushuhudia Bendi ya Mashujaa iliyokuwa ikitumbuiza akifuatana na watu wawili, mmoja mwanaume na mwingine mwanamke.
Inadaiwa kuwa Shilole alipoingia ukumbini humo na kuonana na Ngassa aliyekuwa na kampani yake, alipandwa na hasira na kuanza kujibishana naye.
Chanzo kinatiririka kuwa kabla Shilole hajaingia ukumbini humo, alimuomba kijana anayeuza pipi aitwaye Abdallah Rashid amuoshee gari lake kwani lilikuwa limechafuka bila ya kukubaliana naye bei.
Baada ya Shilole kutoka kwa hasira kutokana na kujibishana na Ngassa, moja kwa moja aliingia kwenye gari lake na kutaka kuondoka bila ya kumlipa kijana aliyemuoshea gari lake.
“Kwani unanidai shilingi ngapi?” Shilole alimuuliza kijana aliyesema kwamba anadai shilingi elfu tano.
“Baada ya Shilole kutajiwa kiasi hicho, alikataa kulipa kwa kuwa ni kikubwa na kumfanya kijana huyo kuwa mbogo na kuanza kurushiana maneno na staa huyo,” kilisema chanzo chetu.
Chanzo hicho kikaendelea kutoboa kuwa wakati kijana huyo akipigizana kelele na Shilole, Ngassa alitokea na kumvaa huku akimuuliza kwa nini anagombana na wanawake na kuanza kurushiana naye maneno, kiasi cha kutaka kuzipiga lakini wakatulizwa na wasamaria wema.
“Ngassa alikunjwa na jamaa ambaye alikuwa amekasirika kutokana na kudhulumiwa haki yake,” kilisema chanzo chetu.
Hata hivyo, baada ya ugomvi huo, Shilole na Ngassa kila mmoja aliingia kwenye gari lake na kutokomea bila kumlipa aliyeosha gari.
Baadhi ya mashuhuda walisema kuwa Ngassa na Shilole walikuwa na ugomvi uliohusiana na masuala ya kimapenzi.
“Hata yule mwanamke aliyekuwa na Ngassa alisema kwamba Shilole anahangaika kumfuata Ngassa wakati mcheza soka huyo hamtaki,” kilisema chanzo chetu.
Paparazi wetu alipompigia simu Ngassa kumuuliza kuhusiana na timbwili hilo, alikiri kutokea na kusema kuwa alikuwa akimsaidia Shilole.
Aidha, Ngassa alikanusha madai ya kuwa na uhusiano wa kimapenzi na Shilole kwa kusema kuwa hawezi kutembea na msanii wa filamu.
Naye Shilole alipopigiwa simu alisema kuwa timbwili lilizuka kati yake na mtu aliyeosha gari lake bila ya ridhaa yake.
“Miye nimeenda pale kimpango wangu wala sikumfuata Ngassa ingawaje kweli nilimuona lakini wala sikuongea naye,” alisema staa wa muziki na filamu.
Huku ikidaiwa ni Wapenzi-Ngasa na Shilole Wazua Timbwili
0
March 21, 2013
Tags