Kampuni za Ndege Lawamani Kuinyima Mapato Swissport


Baadhi ya kanuni zinazosimamia utoaji huduma kwenye viwanja vya ndege hazitekelezwi ipasavyo kutokana na kampuni zingine kukiuka masharti ya leseni zao, imeelezwa.

Kanuni hizo haziruhusu watu wanaotoa huduma ya usafiri wa anga kujihudumia wenyewe, lakini ziko baadhi ya kampuni zimekiuka masharti ya leseni zao na kujihudumia zenyewe.

Akizungumza Dar es Salaam jana wakati wa mkutano wa wadau ulioitishwa na Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA), Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Swissport, Gaudence Temu alisema hali hiyo inawanyima mapato na kuhatarisha uhai wa kampuni zingine.

 “Kwanini sheria zitumike kwa operators (waendeshaji) wengine na kwa wengine zisitumike… tunashauri sheria zifuatwe,” alisema Temu.

Alisema kanuni zinaelekeza ndege zinazochukua abiria 19 kushuka chini, ndizo zinaruhusiwa kujihudumia zenyewe na kuruhusiwa kuingia mkataba na shirika lingine kupeana huduma lakini wapo ambao wanakwenda kinyume na kanuni hizo.

Akizungumzia madai hayo, Mwenyekiti wa bodi ya mamlaka hiyo, Mwatumu Malale alishauri watu wote wenye mapendekezo jinsi ya kuboresha utendaji kuyapeleke kwa maandishi ili yafanyiwe kazi.

Mkurugenzi wa Kampuni ya TanzanAir, Abdukadir Mohamed aliishauri mamlaka hiyo kuangalia uwezekano wa kuajiri vijana wa Tanzania ambao wamehitimu taaluma ya urubani.

“Wengi wana masaa machache, tuangalie jinsi tutawasaidia vijana wetu ili wapate uzoefu na hatimaye kuajiriwa,” alisema Mohamed.

Katika hatua nyingine, mamlaka hiyo imepokea maombi 16 ya leseni kwa ajili ya huduma za usafiri wa anga, upakuaji na upakiaji mizigo na kutoa huduma ya chakula.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad