Kaseja, Yondani wafuatwa na wazungu Dar es Salaam

CHAMA cha Soka nchini Denmark (DBU), kimetuma kikosi kazi cha watu wawili kwa ajili ya kuwafuatilia nyota wa Taifa Stars.
Hatua hiyo inakuja kufuatia Kocha Mkuu wa Stars, Mdenishi Kim Poulsen, kufanya mazungumzo na chama hicho na kukikaribisha nchini kufuatilia maendeleo ya kikosi chake pamoja na timu za vijana ambazo zipo chini ya Jacob Michelsen.
Wageni hao walishuhudiwa na Championi Jumatano wakiwa ‘bize’ kuchukua video za mazoezi ya Taifa Stars yaliyokuwa yakifanyika juzi jioni kwenye Uwanja wa Karume jijini Dar es Salaam, ikiwa ni siku ya pili tangu waanze kazi hiyo.
Wazungu hao walikuwa bize mara kwa mara wakielekeza kamera zao kwa beki wa Yanga Kelvin Yondani na kipa wa Simba Juma Kaseja.
Wakizungumza na Championi Jumatano, Wazungu hao, wote wakiwa ni raia wa Denmark, Jonas Ryefect na Kristian Andersen, wamesema kazi yao kubwa ni kufuatilia maendeleo ya nyota wa Stars na mara baada ya kumalizika kwa mchezo dhidi ya Morocco, watapeleka mikanda hiyo nchini Denmark ambapo itakabidhiwa kwa DBU.
“Kazi hii nadhani itaweza kuwa na maana kubwa kwa wachezaji wa timu ya taifa na Tanzania kwa jumla ambapo viongozi mbalimbali wa timu za soka na hata chama cha soka, wataweza kuangalia viwango vya wachezaji jambo linaloweza kuwapa nafasi ya kuviuza vipaji vyao.
“Lakini pia tunafuatilia maendeleo ya kazi wanazofanya Kim pamoja na Michelsen,” alisema Ryefect huku akiungwa mkono na Andersen.
Wakati wawili hao wakitamka hayo, Kim amesema ni wakati muafaka kwa nyota wa timu yake kujituma zaidi katika mchezo dhidi ya Morocco kwani wataonekana kwa mawakala mbalimbali ambao wanaweza wakawafanyia mipango ya kucheza soka la kulipwa Ulaya.
Mbali na Yondan na Kaseja kikosi hicho pia kina nyota wengine wengi kutoka Simba, Yanga, Azam pamoja na Mtibwa Sugar.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad