Kesi Hizi Dhidi ya TFF Zinatutia Aibu


Kauli ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Soka Tanzania (FAT), sasa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Michael Wambura la kulitaka shirikisho hilo kuwaangukia wadau waliofungua kesi ya kusimamisha Uchaguzi Mkuu wa TFF, haiwezi kupita bila kupingwa.

TFF imefunguliwa kesi mbili, moja Mwanza na nyingine Tanga, zote zikipinga kufanyika kwa uchaguzi mpaka malalamiko ya walalamikaji kupinga kuenguliwa kwenye uchaguzi yatakaposikilizwa.

Wadau wawili wanalalamika kuenguliwa isivyo halali kushiriki kwenye uchaguzi huo, ambao hata hivyo umesimamishwa na Shirikisho la Soka Ulimwenguni (Fifa).

Fifa ilifikia hatua hiyo baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa baadhi ya wadau waliopinga kuondolewa kushiriki uchaguzi wa TFF na sasa shirikisho hilo linatuma wawakilishi wake kuja kutafuta suluhu.

Hata kabla ya ujumbe wa Fifa kuja nchini, Serikali nayo ni kama imeuzuia uchaguzi huo baada ya kutamka kutoitambua katiba iliyotumika katika mchakato mzima wa uchaguzi na kuitaka TFF kufanya upya marekebisho.

Tunaamini, uamuzi wa Serikali kusitisha matumizi ya katiba mpya ya TFF, kesi mbili zilizofunguliwa dhidi ya shirikisho hilo na ujio wa ujumbe wa Fifa kutafuta suluhu, ni ishara kwamba kuna tatizo.

Ifahamike kuwa, hata kama ujumbe wa Fifa unakuja na kumaliza kasoro zilizopo na TFF ikatekeleza agizo la Serikali kufanya marekebisho, bado juhudi hizo hazitakuwa na maana kama kesi zilizopo mahakamani hazitakwisha.

Kauli ya Wambura ya kuitaka TFF kukutakana na wadau waliofungia kesi na kumaliza tofauti nje ya mahakama, ni msingi na kiini kikuu katika kumaliza yale yasiyopendeza kwa mchezo wa soka kupelekwa mahakama za kiraia.

Kwa upande wao TFF, tunajua kinachotokea kwa sasa ni dosari kubwa na hawafurahishwa hata kidogo. Hakiwafurahishi hata wadau wa soka ambao tayari wameanza kuwa na mitazamo tofauti.

Lakini dosari hizi haziwezi kufutika bila kuwapo na juhudi za makusudi kuhakikisha mchezo wa soka hauendi mahakamani. Kinyume chake, ni kukubali kuichafua sifa nzuri ya nchi yetu katika ramani ya soka la kimataifa.

Tunaamini wadau waliokwenda mahakamani hawakufanya hivyo kwa lengo la kulichafua jina la Tanzania, ila kudai haki yao ya msingi wanayoina wanastahili kupata.

Ikumbuke, hata mahakamani kuna Baraza la Usuluhishi au Baraza la Wazee, ambao msingi wa majukumu yao ni kujaribu kutumia busara na kuwashawishi walalamikaji na walalamikiwa ili ikibidi kumaliza kesi nje ya mahakama.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad