Kikwete Aivulia Kofia Azam

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete ameisifu klabu ya Azam FC kwa dhamira yao ya kuendeleza soka nchini hasa katika uwekezaji wa kiufundi.
Rais Kikwete aliyasema hayo jana wakati wa hafla fupi ya uzinduzi wa Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamanzi, Mbande jijini Dar es Salaam.

Alisema, “Nawapongeza Kampuni ya Bakhresa kwa kuendeleza soka nchini kwani mmekuwa mfano kutokana na mfumo mlionao wa kuendeleza vipaji vya soka kuanzia vijana hadi wakubwa.”

“Siyo kwamba ni mafanikio tu, Azam sasa imekuwa kiboko na inaogopewa na vigogo wa Ligi Kuu, kila mmoja akijua ana mechi na Azam anakuwa na hofu,” alisema Kikwete.
Alisema, “Kutokana na hilo nawasifu kwa sababu mmefanikiwa kuvunja ukiritimba wa Simba na Yanga kwani hivi sasa hatujui mkubwa ni nani kwenye ligi.

“Hii ni kutokana na jinsi mlivyowekeza katika ufundi na siyo kamati za ufundi. Ninaposema ufundi namaanisha kocha, wachezaji na mazingira mazuri, lakini zipo timu badala ya ufundi kazi yao ni kuhonga makipa, wachezaji... ili washinde wakija kuiingia kwenye mashindano makubwa mechi ya kwanza au ya pili nje,” alisema Kikwete.

Akizungumzia Uwanja wa Azam, Kikwete alisema ni jambo zuri na mfano kwa wengine huku akitolea mfano wa Ulaya kuwa timu haziwezi kucheza kwenye uwanja wa kuazima. “Sisemi kwamba TFF wazuie, lakini kila timu inatakiwa kuwa na malengo hasa katika hili la uwanja,” alisema Kikwete.

Pia rais Kikwete alikemea suala la ushirikina katika soka na kusema kama ungekuwa na maana basi Afrika ingekuwa ya kwanza katika michuano ya dunia.

“Hakuna ushirikina kwenye michezo kwani kama uchawi ungekuwa unafanya kazi Afrika wangekuwa mabingwa kila siku, tusikekeze kwenye uchawi tuwekeze kwa wachezaji, wachezaji wanatakiwa kulelewa vizuri, walale pazuri, wale vizuri siyo kula chips mayai.” “Kijumla ninawapongeza Azam kutokana na jinsi nilivyojionea mwenyewe, wao wametekeleza kwa vitendo, nimeona vifaa, gym, bwawa la kuogelea, vyumba vya kulala na kila kitu safi,” alisema Kikwete.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad