Kocha wa Morocco Aongea "Sinta Wasahau Kiemba na Thomas Ulimwengu"


KOCHA Msaidizi wa Morocco, Rachid Bin Mahmoud, amechukizwa na kipigo ilichopata timu yake, lakini akatamka hatawasahau kiungo Amri Kiemba na mshambuliaji Thomas Ulimwengu.

Amri Kiemba.

Kauli hiyo ya Mahmoud inakuja kufuatia Morocco kukubali kichapo cha mabao 3-1 dhidi ya wenyeji wao Taifa Stars katika mchezo wa kuwania nafasi ya kushiriki Fainali za Kombe la Dunia mwakani uliofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na Championi Jumatano, Mahmoud alisema Kiemba alikuwa tatizo kubwa kwa viungo wa timu yake (Morocco) ambapo aliweza kuwaongoza vyema wenzake katika kutibua mipango mingi ya wachezaji wake, jambo ambalo liliwapa wepesi Stars.
Mahmoud ambaye alionekana kuwa na hasira kwa kukunja uso, alisema mbali na Kiemba, pia kuingia kwa Ulimwengu lilikuwa pigo kubwa kwa kikosi chake ambapo mshambuliaji huyo alionekana kuwa na nguvu zaidi akijua upungufu wa mabeki wake na kutoa mchango mkubwa katika ushindi wa mabao hayo.
“Tumefungwa mechi ambayo hatukutarajia, hakuna tunayeweza kumlaumu katika hili lakini yule mchezaji mwenye jezi namba tisa (Kiemba) alikuwa na uwezo mkubwa, alifanikiwa kutibua kila kitu cha timu yetu,” alisema Mahmoud na kuongeza:
 “Ukiachana na huyo, yule mshambuliaji mwenye jezi namba kumi na moja (Ulimwengu) alitupa tabu tangu mwanzo alivyoingia, alikuwa na msaada mkubwa sana, mabeki wetu walishindwa kumdhibiti, lakini ndiyo mpira, nafikiri tunatakiwa kujifunza na tutawadhibiti katika mchezo wa marudiano.”

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad