Dar es Salaam. Kesi inayowakabili Mkuu wa Ulinzi na Usalama wa Chadema, Wilfred Lwakatare na mwenzake Joseph Ludovick Rwezaura imechukua sura mpya kutokana mawakili wanaomtetea kiongozi huyo na mwenzake kupeleka suala hilo Mahakama Kuu.
Mmoja wa wanasheria watano wanaowatetea Lwakatare na mwenzake, Tundu Lissu akizungumza na waandishi wa habari jana alisema hatua yao ya kwe nda Mahakama Kuu inatokana na ukweli kwamba Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) ameingilia uhuru wa Mahakama bila sababu za msingi.
Mbali na Lissu, mawakili wengine wanaomtetea Lwakatare ni Peter Kibatala, Mabere Marando, Abdallah Safari na Nyaronyo Kicheere.
Juzi, Lwakatare na Ludovick walifutiwa mashtaka ya ugaidi yaliyokuwa yakiwakabili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kuachiwa huru, lakini hapohapo wakisha kukamatwa tena na kusomewa mashtaka yaleyale ya awali.
Juzi waliposomewa mashtaka upya, watuhumiwa hao hawakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa Mahakama ya Kisutu haina mamlaka ya kusikiliza kesi za ugaidi, tofauti na Jumatatu waliposomewa mashtaka kwa mara ya kwanza ambapo walipewa fursa ya kukubali au kuyakana mashtaka hayo.
Kwa kuzingatia mazingira hayo, Lissu alisema katika maombi yao watakayoyawasilisha leo Mahakama Kuu, wataiomba iingilie kati mchakato huo ambao wanasema kimsingi unakiuka sheria.