Maandamano ya Mnyika Yakwama


MAANDAMANO yaliyoandaliwa na Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (CHADEMA), yamegonga mwamba kutokana na kuahirishwa, baada ya askari polisi waliokuwa na mabomu ya machozi kuyazuia.

Licha ya askari hao kuzuia maandamano hayo waliruhusu mbunge huyo kuhutubia wananchi waliofika eneo la Manzese, Bakheresa.

Tanzania Daima ilishuhudia wananchi wakirushiana maneno mara kwa mara na askari waliokuwepo katika eneo hilo.

Askari hao wa kutuliza ghasia walikuwa katika gari namba PT 1524, PT 0890, M 672 CAH na PT 1902.

Katika hali isiyo ya kawaida askari mmoja alisikika akiwaambia wananchi waondoke katika eneo hilo, kwani mabomu yakianza kurushwa watawavunja miguu, wakati huo mbunge akiwa anaendelea kula kuku kwa kuwa atakuwa hajaumia.

“Kwanza tunawachelewesha nini hawa tuwavuruge tu,” alisikika askari huyo akisema.

Akihutubia mkutano huo, Mnyika alisema kuwa ni lazima hoja inayohusu masuala ya maji ipatiwe ufumbuzi.

“Leo hatutaandamana, lakini maandamano yatakuwepo baada ya kuwasilisha barua ya kukata rufaa kwa Waziri Nchimbi na tutataka kauli zao,” alisema.

Mnyika alisema kuwa Machi 18, mwaka huu atapeleka barua ya kukata rufaa ya kuzuia maandamano ambapo watahitaji kauli za mawaziri hao kutolewa hadi ifikapo Machi 22, kabla hawajaamua kuandamana tena.

Mnyika pia aliwataka wananchi hao kuhakikisha wanaomba kujiunga na mabaraza ya katiba ili kupata wawakilishi bora watakaoongoza ikiwamo kuhakikisha Katiba mpya na bora itakayotetea masilahi ya wananchi inapatikana.

“Tuombe kushiriki katika mabaraza ya katiba ili tupate katiba itakayohakikisha haki za msingi zinalindwa,” alisema.

Awali Kamanda wa Polisi wa Wilaya ya Kinondoni, ACP Charles Kenyela, alikataza maandamano na mkutano huo, ambapo alitoa sababu mbalimbali ikiwamo eneo hilo la Manzese Bakhresa kutumika kwa maegesho ya magari ya mizigo.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad