Nairobi. Mahakama ya Juu (Supreme Court) ya nchini Kenya imeagiza kuchunguzwa kwa fomu 34 za matokeo ya uchaguzi wa rais kutoka katika vituo vyote 34,400, vilivyotumika kupigia kura katika Uchaguzi Mkuu wa nchi hiyo uliofanyika Machi 4, mwaka huu.
Kadhalika mahakama hiyo jana iliagiza kuhesabiwa upya kwa kura za urais katika vituo vya kupigia kura 22 kati ya elfu 33 vilivyolalamikiwa na aliyekuwa mgombea urais wa Muungano wa Cord, Raila Odinga.
Katika malalamiko yake yaliyowasilishwa katika mahakama hiyo kupinga Uhuru Kenyatta kutangazwa mshindi wa urais katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Machi 4, Odinga alidai kuwa vituo hivyo 22 kura zilizopigwa zinazidi idadi ya wapigakura walioandikishwa.
Akisoma uamuzi huo kwa niaba ya majaji wenzake watano, Jaji Smokin Wanjala alisema kwamba uhesabuji kura wa vituo hivyo utafanyika leo kuanzia saa 2.00 asubuhi kwa lengo la kubaini ukweli kuhusu madai hayo.
“Matokeo ya kura zitakazohesabiwa katika vituo hivyo 22 yawasilishwe katika mahakama hii Jumatano, saa 10.00 jioni,” alisema Jaji Wanjala.
Kikao hicho, ambacho Jaji Mkuu wa Tanzania, Mohamed Othman Chande amealikwa kama mwangalizi, ni cha awali kabla ya kesi hiyo kuanza kusikilizwa rasmi keshokutwa (Alhamisi) na kuendelea kwa mfululizo hadi kufikia uamuzi ikiwa madhumuni yake.
Lengo ni kupitia madai yaliyowasilishwa mahakamani hapo na pande zote zinazohusika na kuamua mwenendo wa kesi utakavyofanyika.
Source:Mwananchi
Mahakama yaamuru matokeo ya urais Kenya yachunguzwe
2
March 26, 2013
Tags
Sisi Raisi wetu wa Kenya twamjua tayari na bado kuapishwa tu.
ReplyDeleteNi muhimu sana haki iende kwa mwenye haki, na Mungu atatunusuru, sema Amen
ReplyDelete