MKURUGENZI wa zamani wa Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (Tanesco) aliyefukuzwa kazi kwa tuhuma za ufisadi, William Mhando, yamemkuta baada ya mtu mmoja aliyejitambulisha kuwa ni mchungaji kumliza magari matano.
Vyanzo vyetu vya habari ndani ya jeshi la polisi vinadai kwamba, Mhando alitinga Kituo cha Polisi cha Oysterbay na kufungua kesi na OB/RB/3394 inayohusiana na wizi hivi karibuni.
Taarifa zaidi zinaeleza kwamba, Mhando alitapeliwa magari hayo Januari 30, mwaka huu na mtu aliyejulikana kwa jina la Mchungaji Joseph anayedaiwa kuwa anahudumu katika kanisa moja huko Kigamboni wilayani Temeke jijini Dar es Salaam.
Habari zilizopatikana Kituo cha Polisi Oysterbay zinadai kuwa, magari yaliyokodishwa kwa ajili ya kuwasafirisha wanafunzi kwenda kutalii ni aina ya Prado, Nissan Ribert,Rav 4 mbili hadi leo hii hayajaonekana wala mchungaji huyo hajaonekana.
“Polisi wa hapa Oysterbay wanaendelea kufanya uchunguzi wa kina kwa sababu magari hayo huenda yameshauzwa na aliyeyakodisha,” alisema askari mmoja ambaye hakutaka jina lake litajwe.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, ACP Charles Kenyela alithibitisha kuwepo kwa sakata hilo lakini akasema hajapata taarifa kutoka kwa maofisa wake wanaoshughulikia suala hilo.
William Mhando alipotafutwa kwa njia ya simu ya kiganjani hakuweza kupatikana kwani ilikuwa ikiita bila kupokelewa.