Muhidin Ndolanga Awapiga Dongo TFF

Mjumbe wa Heshima wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Muhidin Ndolanga amelitupia lawama shirikisho hilo, akisema linahusika moja kwa moja ‘kutengeneza’ mgogoro alioutafsiri kuwa una dhamira ya masilahi binafsi kwa baadhi ya watu, hatua iliyopelekea kukwaruzana na serikali.

Aidha, amesema uamuzi wa serikali kuingilia kati utendaji wa shirikisho hilo ni sahihi kwa vile kinachoendelea ndani ya TFF, siyo tu kwamba hakikubali, bali pia hakivumili na wadau wengi wa soka. Akizungumza na gazeti hili jana, Ndolanga alisema taswira ya sasa TFF, ni uroho wa madaraka kwa baadhi ya watu ambao hawako tayari kuona mabadiliko makubwa yanafanyika.

Shirikisho la Soka Duniani (Fifa), tayari limeshaonya kuwa Tanzania inaweza kufungiwa iwapo itabainika kuwa serikali inaingilia kati utendaji wa TFF.

“Fifa haiwezi kutoa onyo bila TFF kulalamika. Kuna mtu amepeleka taarifa Fifa. Ndani ya TFF kuna watu wanafanya kazi kwa woga. Kama ningekuwa mimi (Ndolanga), ningesema wazi nahusika kuwajulisha Fifa na ningetoa sababu.

“Haiwezekani TFF ifanye madudu katika utendaji wake na bado itegemee watu wakae kimya. Yaani dhambi na dhuluma ziachwe hivihivi, kisa Fifa watatufungia...,” alisema Ndolanga ambaye enzi ya utawala wa kilichokuwa Chama cha Soka (FAT), Tanzania iliwahi kufungia kwa sababu ya serikali kuingilia kati utendaji wake”

Aliongeza: “Binafsi sioni mahali serikali ilipofanya makosa mpaka sasa. Ingefanya makosa mimi siogopi lazima ningeikosoa, ningesema hili hapana---mmekosea.
Muda wa kukaa madarakani kwa Tenga na timu yake umekwisha, walitakiwa wapangilie mambo yao mapema ikifika Desemba 31 waondoke waache uongozi mpya.”

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad