Moshi. Polisi mkoani Kilimanjaro, wamemtia mbaroni mtu mmoja mjini Moshi, kwa tuhuma za kuzalisha kienyeji soda za jamii ya Cocacola, zinazozalishwa na Kiwanda cha Bonite Bottlers Ltd.
Kiwanda hicho kinamilikiwa na Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Reginald Mengi na kinazalisha soda mbalimbali zikiwamo Fanta, Cocacola, Krest, Sparlleta, Sprite na Stone Tangawizi.
Mtuhumiwa huyo mkazi wa Kibosho Kindi Kibaoni, Moshi Vijijini, alikamatwa juzi usiku katika operesheni ya polisi wakishirikiana na maofisa usalama wa kiwanda hicho.
Habari zilizothibitishwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz zilisema mtuhumiwa pia alikutwa na masanduku sita ya soda alizokuwa amezitengeneza na masanduku 11 ya chupa za soda kubwa.
Alisema katika upekuzi katika nyumba ya mtuhumiwa, polisi walikuta masanduku zaidi ya 400 ya chupa tupu za soda ya jamii ya Cocacola.
“Tulimkuta anazalisha soda za jamii ya Cocacola nyumbani kwake. Kuna wakati alikuwa akichukua soda zilizomo kwenye chupa kubwa anazijaza kienyeji kwenye chupa ndogo,”alisema Kamanda Boaz.
Kwa mujibu wa Kamanda Boaz, mtuhumiwa huyo pia alikuwa akichukua soda za unga zilizopo katika paketi na kuzichanganya kwenye maji na kisha kuzijaza kienyeji kwenye chupa za jamii ya Cocacola.