Matukio yanayoendelea kutokea katika nchi yetu yanaonyesha
pasipo shaka kuwa, iwapo Serikali haitachukua hatua za haraka na za
makusudi, Tanzania itakuwa moja ya nchi zinazojulikana kwa vitendo vya
kimafya. Mbali na matukio ya vurugu za kidini katika baadhi ya sehemu
za nchi ambayo tayari yamedhibitiwa, sasa yamejitokeza matukio kadhaa
tunayoweza kuyaita ya kimafya.
Matukio kama hayo hutokea katika nchi zisizo na serikali au zenye serikali legelege. Katika nchi hizo, hujitokeza makundi ya kihalifu yenye kufuata sheria za msituni na kujipa mamlaka ya kuunda mfumo wake wa kihalifu kama biashara ya madawa ya kulevya, wakati mwingine kwa ushirikiano na vyombo vya dola. Ushirikiano huo huyawezesha makundi hayo kupata silaha, fedha na taarifa muhimu kuhusu kinachojiri ndani ya serikali husika.