TCRA Yagoma Kata Kata Kurudisha Mfumo wa Zamani wa Analogia


Dar es Salaam. Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imesema haitarudi nyuma kwenye suala la kutumia mfumo wa matangazo kupitia njia ya dijitali na kwamba mfumo huo utaendelea kutumika.


Kauli ya TCRA imekuja siku moja baada ya wamiliki wa vituo vya utangazaji vya televisheni nchini kutishia kusitisha kurusha matangazo ndani ya mwezi mmoja kuanzia sasa kutokana na kushindwa kumudu gharama za uendeshaji.


Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania (Moat), Reginald Mengi juzi alisema hakuna haja ya kurusha matangazo kwa hasara kwani watangazaji wamesitisha kutoa matangazo kwa sababu wananchi wengi hawana ving’amuzi. Licha ya Moat kutoa kauli hiyo juzi, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Profesa John Nkoma alisisitiza kwamba TCRA haiwezi kurudi nyuma katika suala hilo kwani mfumo huo utaendelea kutumika.


Akizungumza Dar es Salaam jana kwenye warsha ya mambo ya mionzi, alisema wao kama TCRA hawawezi kurudi nyuma katika suala hilo na kwamba msimamo wao wa kuendelea kutumia mfumo wa matangazo kwa njia ya dijitali upo palepale.


“Sikiliza niwaambie waandishi, leo tupo hapa kwa suala moja la mambo ya mionzi, lakini kwa ufupi ni kwamba sisi hatuwezi kurudi nyuma katika suala hilo la mfumo wa dijitali,” alisema Profesa Nkoma.


Alisema ili kuelezea jambo hilo kwa undani watafanya warsha ya kuzungumzia mambo hayo na kwamba hapo kila kitu kitaelezwa kwa kina.


“Tutafanya warsha kueleza mambo hayo yote na nyie pia kama waandishi mtaelezwa kila kitu, lakini kwa sasa naomba tuyaache kama yalivyo,” alisema.


TCRA ilizima mitambo ya analojia na kuhamia dijitali, Desemba 31, mwaka jana kitendo ambacho Moat wanadai kimepunguza mapato yanayotokana na matangazo.

Post a Comment

2 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. inchi ishauzwa hii.tutanyonywa damu na serikali mpaka tutapokwenda kaburini ndo unafuu wetu.

    ReplyDelete
  2. vng'amuz ni kimradi wamejiwekea..so ni vgumu kukiachia

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad