Ukosefu wa walimu, upungufu wa vitabu na mazingira duni ya kujifunzia, ni baadhi ya sababu zilizotolewa kwa wingi na wadau wa elimu waliohojiwa na Tume ya Kuchunguza Matokeo ya Kidato cha Nne mwaka 2012 iliyoundwa na Waziri Mkuu.
Hayo yalielezwa jana na Mwenyekiti wa tume hiyo, Profesa Sifuni Mchome alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
“Watu wengi wanasema sababu za matokeo kuwa mabaya ni shida ya walimu, vitabu vichache na vingine vimepitwa na wakati, wanazungumzia pia usimamiaji wa shule na ukaguzi,” alisema Profesa Mchome.
Profesa Mchome alitaja sababu nyingine zinazotolewa kuwa ni pamoja na shule nyingi kutokuwa na mabweni pamoja na miundombinu mibovu ya kujifunzia.
Profesa Mchome alisema kuwa, maelezo hayo ni kutoka kwa wadau mbalimbali waliotembelea kwenye tume hiyo, kutuma baruapepe, maandiko ama kutoa maoni kupitia kwenye tovuti ya tume hiyo.
“Pia wapo waliozungumza kwenye shule 26 za Mkoa wa Dar es Salaam ambazo wajumbe walizitembelea kuzungumza na walimu, wajumbe wa bodi za shule na wanafunzi,” alisema Profesa Mchome.
Alibainisha kuwa, katika kila shule waliyotembelea walizungumza na watu wasiopungua 40, ambao kwa ujumla wake alisema walitoa maoni mazuri.
Profesa Mchome alifafanua kuwa, kwa sasa wajumbe wa tume hiyo wapo mikoani wakizungunza na wadau mbalimbali ili kuweza kupata sababu ya matokeo mabovu.
Alisema kuwa wananchi wajitokeze kwa wingi ili kuweza kutoa maoni juu ya sababu zinazokwamisha elimu nchini.
Profesa Mchome alisema kuwa, mpaka sasa maelfu ya watu wametoa maoni yao kwa njia mbalimbali ikiwamo kufika moja kwa moja katika ofisi za tume, kupitia tovuti ya tume, baruapepe, kuandika maandiko mbalimbali pamoja na kufika kutuma ujumbe mfupi wa simu.
Alisema tayari tume yake imezungumza na makundi 12 ya wadau mbalimbali wa elimu yakiwamo ya Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Wamiliki wa Shule Binafsi (TAMONGSCO), Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) na Baraza la Mitihani la Taifa (Necta)
Hata hivyo alisisitiza kwamba mahojiano ya Necta na Tet ni ya awali. Kwa sasa wajumbe wako katika mikoa ya Lindi, Mtwara, Tanga, Manyara, Arusha, Morogoro, Pwani, Simiyu, Shinyanga, Mbeya na kati ya Machi 24 na 26 watakuwa katika Mkoa wa Dodoma, Unguja na Pemba.