Wakati Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), ikiwataka
wananchi wa Kenya kuwa na subira wakati ikiendelea kukusanya na kuhesabu
kura, mgombea wa Jubilee, Uhuru Kenyata anaendelea kuongoza kwa kura
dhidi ya mgombea wa Muungano wa Cord, Raila Odinga.
Tangu kura zianze kuhesabiwa juzi jioni, Kenyatta amekuwa akiongoza wagombea wengine wa urais katika uchaguzi huo.
Tamko la Mwenyekiti wa IEBC, Isaack Hassan jana
asubuhi lilitokana na malalamiko yaliyoanza kutolewa na wananchi na
vyama vya siasa vilivyoshiriki uchaguzi huo kuwa matokeo
yanacheleweshwa.
IEBC ilikuwa imeahidi kutangaza matokeo ya urais
ndani ya saa 48 baada ya kufungwa kwa vituo vya kupigia kura juzi saa 11
jioni hakukuwa na matokeo hayo.
Kwa siku nzima jana, matokeo ya awali yaliendelea
kutolewa lakini kwa kasi ndogo ikilinganishwa na juzi, huku mgombea
urais kupitia Jubilee, Uhuru Kenyatta akiongoza akiwa na kura 2,735,353
(53.49%) dhidi ya Raila Odinga wa Cord aliyekuwa na 2,145,721 (41.96%)
hadi kufikia saa 1 jioni jana.
Hassan alisema matokeo hayo yalichelewa kutokana
na matatizo yaliyojitokeza ya baadhi ya mashine za utambuzi wa
wapigakura kukwama na kusuasua kwa mtandao (network down) juzi usiku.
Aliwataka wananchi kuwa watulivu na wavumilivu
wakati wakiendelea kupokea matokeo ya awali, kwa kuwa matokeo rasmi
yangesubiri wasimamizi kuwasili Nairobi kutoka mikoani, wakiwa na
karatasi rasmi za matokeo kwa ajili ya kulinganisha, hatua ambayo
alisema isingewezekana ndani ya saa 48.
Alisema wasimamizi kutoka katika majimbo 290 na
kaunti 47 walikuwa safarini kutoka mikoani kwenda Nairobi, hatua ambayo
ingesaidia tangazo rasmi la matokeo.
“Tunatarajia wafike mchana wa leo (jana),” alisema
Hassan alipozungumza na waandishi wa habari katika kituo cha
kujumlishia kura, Bomas.
Hassan alitupilia mbali madai ya Muungano wa Cord
kuwa matokeo hayo yanacheleweshwa akisema hayana msingi kwa kuwa sheria
ya uchaguzi inaruhusu matokeo kutangazwa ndani ya siku saba, hivyo
alikuwa bado na siku sita mkononi kisheria.
Alitumia nafasi hiyo kuzima furaha ya baadhi ya watu: “Hadi sasa tumepata matokeo kutoka vituo 23,000 kwa nchi nzima.
Hakuna anayestahili kushangilia, hakuna
anayestahili kulalamika. Huu siyo muda wa kushangilia wala kuhuzunika,”
alisema Hassan. Katika uchaguzi huo kulikuwa na vituo 31,981.
Alisema hawawezi kurudia makosa yaliyofanywa na iliyokuwa Tume ya Uchaguzi (ECK), mwaka 2007 yaliyoharibu uchaguzi na kusababisha machafuko.
Alisema hawawezi kurudia makosa yaliyofanywa na iliyokuwa Tume ya Uchaguzi (ECK), mwaka 2007 yaliyoharibu uchaguzi na kusababisha machafuko.