Yanga Yaipoteza Simba


Baada ya kumaliza Ligi Kuu msimu uliopita katika nafasi ya tatu, kwa mara ya kwanza baada ya miaka mingi ya historia ya ligi, Yanga sasa ipo mbioni kunyakuwa taji lake la 23 msimu huu.

Ikiwa inaongoza kwa tofauti ya sita dhidi ya timu inayoshika nafasi ya pili kwenye msimamo, Azam FC na pointi 11 dhidi ya mabingwa watetezi, Simba vijana hao wa Jangwani wameonyesha dhamira kuwapokonya taji mahasimu wao.

Kasi ya Yanga msimu huu imekua gumzo kutokana na kushinda mechi mfululizo, ambapo mwishoni mwa wiki iliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Kagera Sugar, na ushindi kama huo katika mchezo uliotangulia dhidi ya Azam.

Wakati Simba ilipokuwa ikiongoza msimamo wa ligi katika raundi tano za kwanza duru la kwanza, Yanga ilikuwa inaburuza mkia ikiwa ni mara ya kwanza katika kipindi cha zaidi ya miaka 20 kushika nafasi hiyo.

Hata hivyo, wakati duru wa kwanza ukimalizika mwishoni mwa mwaka jana, tayari Yanga ilisharudi kileleni na kuongoza ligi mpaka sasa na kuzidi kuziacha Simba na Azam katika vita ya kuwania nafasi ya pili.

Lakini safari hii Yanga wamepania kuhakikisha wanapanda ndege na kushiriki Ligi ya mabingwa Afrika mapema mwakani kwani tangu kuanza kwa msimu walisajili vizuri na timu yao imeonyesha kiwango kinachotamanisha.

Yanga inaongoza baada ya kucheza michezo 18, imeshinda 13, imetoa sare  mitatu, imepoteza miwili ina magoli 35 ya kufungwa na imefungwa 12, wakati mabingwa watetezi, Simba wakiwa nafasi ya tatu na pointi 31 baada ya mechi 18, wakishinda nane, sare saba, kupoteza mitatu wamefunga 26 na kufungwa 15. Azam wako nafasi ya pili wakiwa na pointi 36, wamecheza michezo 18, wameshinda 11, wametoa sare  mitatu, wamepoteza minne, wamefunga magoli 31 na wamefungwa 15.

Timu hizo zote tatu zimebakisha mechi nane kabla ya msimu kufungwa rasmi, huku Coastal Union ikionekana kujiimarisha katika mbio za kuwania nafasi za juu ikilingana kwa pointi na Simba.
Kama dhamira ya Simba kutwaa ubingwa msimu huu itabaki palepale, watalazimika kusali ili Yanga ipoteze mechi tano kati ya nane zilizobaki na wao kushinda mechi zao.

Ikiwa Yanga atafungwa mechi tano na kushinda tatu atafikisha pointi 51, wakati Azam akifungwa mechi nne na kushinda nne, atafikisha pointi 48 wakati Simba akishinda mechi saba na hata akifungwa moja atafikisha pointi 52 na kutwaa ubingwa.

Lakini kama Yanga atashinda mechi zote ikiwemo dhidi ya Simba basi atafikisha pointi 66, ambazo haziwezi kufikiwa na Azam hata kama atashinda  mechi zote ikiwemo dhidi ya Simba kwani atakuwa amefikisha pointi 60.

Hata kama Simba itashinda mechi zote ikiwemo dhidi ya Azam na Yanga itakuwa na pointi 55, na hazitawasaidia ikiwa Yanga na Azam zitashinda mechi zao saba.

Simba ni lazima washinde mechi zao ngumu dhidi ya Coastal Union (Machi 10, Dar), Kagera Sugar (Machi 27, Kaitaba), Toto (Machi 30, Mwanza), Azam (April 13, Dar) na Yanga (Mei 18, Dar).

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad