Serikali imesema itarudisha adhabu ya viboko kwa wanafunzi shuleni ili kujenga nidhamu na kujituma.Akizungumza Dar es Salaam jana wakati akizindua tovuti ya www.shledirect.co.tz inayowezesha wanafunzi kujisomea kwa njia ya mtandao, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo ilisema kuondolewa kwa adhabu ya viboko shuleni kumewafanya wanafunzi wengi kukosa nidhamu na wakati mwingine kujifanyia mambo kienyeji.
“Wasipotandikwa mambo hayaendi, nilipokuwa mwalimu mkuu nilikuwa nawatandika kweli ndiyo maana shule yangu ilikuwa ikiongoza Mkoa wa Mbeya hivihivi hawaendi...” alisema huku akishangiliwa na wageni waalikwa.
Alisema watoto wa siku hizi wamekuwa wakitumia vibaya teknolojia ambayo ingeweza kuwasaidia kwa kiasi kikubwa katika masomo yao... “Tovuti kama hiyo ingewasaidia kwa masomo, lakini wao wanakimbilia kwenye facebook na mambo mengine yasiyofaa.”
Aliyalaumu mashirika yasiyo ya kiserikali na haki za binadamu ambayo yamekuwa yakipigania kuondolewa kwa adhabu hiyo shuleni na kusababisha kushuka kwa nidhamu kwa kiasi kikubwa.
Kadhalika alisema Serikali imepiga marufuku matumizi ya simu za mikononi kwa sababu baadhi ya wanafunzi wamekuwa wakizitumia vibaya jambo ambalo linawarudisha nyuma kimasomo.
“Simu tunazipiga marufuku, mwalimu akimkuta mwanafunzi na simu amnyang’anye ndizo zinatuharibia taifa letu.”