Kocha wa Azam FC, Stewart Hall amesema yupo tayari kuwapokea kwa mikono miwili wachezaji wake wanne ambao Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imeshindwa kuthibitisha tuhuma zao za kupokea rushwa.
Jana,Takukuru kupitia kwa Ofisa Uhusiano wake, Doreen Kapwani ilitoa taarifa kwa vyombo vya habari ikieleza kuwa imeshindwa kuthibitisha tuhuma za rushwa dhidi ya wachezaji wa Azam, Aggrey Morris, Erasto Nyoni, Deogratias Munishi na Said Mourad.
Awali, uongoni wa Azam uliwasimamisha wachezaji hao ukiwatuhumu kupokea rushwa ya Sh 7 milioni na kugawana kwa lengo la kupanga matokeo ya mechi kati ya Azam na Simba iliyochezwa Oktoba 27 mwaka jana.
Kwa mujibu wa Takukuru, fedha hizo zilidaiwa kupokewa siku moja kabla ya mechi kati ya timu hiyo na Simba.
Akizungumza na gazei hili jana Hall alisema: “Kwanza naomba nieleweke mimi si mwanasiasa, mimi ni mtaalamu, kifupi nawakaribisha kwa mikono miwili kwani ni wachezaji wazuri na muhimu ambao watanisaidia kutengeneza kikosi imara. “Pamoja na hayo, uongozi ndio uliwasimamisha si mimi hivyo uamuzi wa mwisho wa kuwarudisha kikosini au ala ni wao.”
Mwenyekiti wa Azam, Said Mohamed alipotafutwa kuzungumzia suala hilo alisema: ”Naomba mambo ya mpira tuyaache kwanza, nipo kwenye mkutano.”
Kwa upande wao Morris na Nyoni walipotafutwa kuzungumzia uamuzi huo wa Takukuru walidai kufurahishwa na kusema kuwa ulikuwa wa haki kwa vile tuhuma dhidi yao hazikuwa na ukweli wowote.
Awali, Kapwani alitoa wito kwa taasisi na wananchi kuendelea kutoa taarifa za tuhuma za rushwa kwa taasisi hiyo ili ziweze kufanyiwa kazi kwa lengo la kudhibiti vitendo vya rushwa.
“Kosa la kupokea rushwa ni kinyume na Kifungu cha 15(1) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 11 ya mwaka 2007, Azam imetimiza wajibu wake wa kushiriki katika kuzuia na kupambana na rushwa hivyo ni wajibu wa taasisi nyingine na wananchi kuendelea kutoa taarifa ili vitendo hivi viweze kudhibitiwa,”alisema Kapwani katika taarifa yake.