Kufuru Msiba wa Bilionea Sambeke
0
April 16, 2013
Arusha. Wakati mazishi ya mfanyabiashara bilionea wa Moshi, Ernest Babu ‘Sambeke’ yakiwa yamepangwa kufanyika keshokutwa, msiba wake umekuwa wa kitajiri kutokana vyakula na vinywaji kumwagwa kwa wingi nyumbani kwa marehemu.
Msiba wa mfanyabiashara huyo uko nyumbani kwake, Njiro – Themi nje kidogo wa Mji wa Arusha ambako habari zinasema mamia ya watu wamekuwa wakifurika kuhani.
Matajiri wa Mikoa ya Kilimanjaro na Arusha wakiwa na magari ya kifahari wamefurika katika msiba huo na habari zaidi zinasema mamilioni ya shilingi yamechangwa kwa ajili ya kufanikisha mazishi ya bilionea huyo aliyefariki dunia, Jumamosi iliyopita kwenye ajali ya ndege.
Ajali hiyo ilitokana na ndege aina ya MT 7- yenye namba 5H-QTT ambayo alikuwa akiiendesha mwenyewe kuanguka kwenye Uwanja wa Ndege wa Arusha, baada ya bawa lake kugonga mti katika eneo la Magereza linalopakana na uwanja huo.
Alifariki dunia wakati askari magereza waliompa msaada walipokuwa wakimkimbiza hosipitali kwa ajili ya kupatiwa matibabu kutokana na majeraha makubwa aliyoyapata kichwani.
Meneja wa Uwanja wa Ndege Arusha, Ester Dede alisema uchunguzi wa ajali hiyo unaendelea kufanywa na wataalamu wawili wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga kutoka Dar es Salaam.
Tags