Lissu afichua mapya sakata la Lwakatare


Mwanasheria wa CHADEMA,Tundu Lissu, amesema wamebaini kuwepo kwa mawasiliano zaidi kati ya Mwigulu Nchemba na mtuhumiwa mwenza wa Lwakatare, aitwaye Ludovick Joseph.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Lissu alidai kuwa tarehe Januari 14, mwaka huu, namba ya simu+255756008888- ya Nchemba inayoonekana kwenye kitabu cha mawasiliano ya wabunge ilituma kiasi cha sh 50,000 kwenda kwa Ludovick.

“Mtakumbuka kuwa video hiyo inayodaiwa kuwa ya kupanga ugaidi ilichukuliwa Desemba 28 mwaka jana, siku moja baadaye Nchemba, kupitia kituo cha Star tv alitangaza kuwa anayo CD ya viongozi wa CHADEMA wakipanga mauaji na akarudia tena Jabuari 2 mwaka huu.

“Sasa tunajiuliza Naibu Katibu Mkuu wa CCM alikuwa na biashara gani na mtuhumiwa wa ugaidi Ludovick, ikizingatiwa pia kuwa siku hiyo hiyo ambayo mkanda ulichukuliwa waliongea kwenye simu?!” alisema Lissu.

Aliongeza kuwa kuna njama kubwa alizodai zinapangwa na dola ili Lwakatare athibitike kuwa alifanya matendo ya kigaidi na hatimaye ionekane kuwa chama anachokitumikia kama Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama kinajihusisha na ugaidi.

Aliongeza kuwa Kamati Kuu ya CHADEMA imejadili kwa kina suala la Lwakatare na kuamua kuwa masuala yote yanayohusu njama dhidi yao kupitia sakata la Lwakatare ni muhimu yawekwe wazi hadharani kadiri inavyowezekana ili Watanzania wajue hujuma dhidi ya chama hicho.

“Napenda kurudia hekaheka zinazoonekana sasa kupitia hata vyombo vya habari kama vile magazeti kuwa CHADEMA inahusika na ugaidi na kupanga njama za mauaji, ni mwendelezo wa propaganda,” alisema Lissu.

Katika mlolongo wa madai hayo, Lissu alisema pia kuwa chama hicho kimebaini kuwepo kwa mawasiliano ya mara kwa mara kati ya Ludovick na mtu aitwaye Dennis Msaki ambaye kwa mujibu wa jalada la polisi katika hati ya mashtaka ndiye anadaiwa kupangiwa njama za kutekwa na Lwakatare na Ludovick.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad