Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema kwa gharama yoyote kipo tayari kumtetea Mkurugenzi wake wa Ulinzi na Usalama, Wilfred Lwakatare dhidi ya kesi ya ugaidi inayomkabili.
Lwakatare na mwenzake, Joseph Rwezaura, wanakabiliwa na kesi ya ugaidi katika Mahakama ya Kisutu, wakikabiliwa na mashtaka manne ya kula njama na kufanya mipango ya kumteka, kisha kumdhuru kwa sumu, Mhariri Mtendaji wa gazeti la Mwananchi, Dennis Msacky.
Majalada hayo namba 37 na namba 6 yote ya mwaka 2013, yalishawasilishwa Mahakama Kuu, kwa awamu mbili. Jalada la kwanza, namba 37 liliwasilishwa Mahakama Kuu, Jumatatu na jalada la pili namba 6 liliwasilishwa Jumanne wiki hii iliyopita.
Mkurugenzi wa Sheria na Haki za Binadamu wa Chadema, Tundu Lissu alisema kuna wanaohoji nguvu ya kisheria wanayoitumia kuweka jopo la mawakili watano kumtetea Lwakatare, akisisitiza kuwa wapo tayari kuhakikisha sheria inatumika ipasavyo kubainisha ukweli wa tuhuma hizo.
Lissu aliyasema hayo jana alipokuwa akieleza msimamo wa baadhi ya mambo yaliyojadiliwa na Kamati Kuu kwenye kikao chake kilichofanyika Dar es Salaam.
Pia, alisema wanamwamini Jaji Lawrence Kaduri aliyepangwa kusikiliza maombi ya kupinga utaratibu wa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP). “Jaji Kaduri aliyepangwa kusikiliza kesi hii aliwahi kuwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) miaka kadhaa iliyopita, hivyo tunaamini kwa uzoefu wake alionao kwenye masuala ya sheria ataamua kwa kuzingatia sheria,” alisema.