Mtandao hatari: Washirika wa Ludovick waanza kubainika
1
April 17, 2013
*Washirika wa Ludovick waanza kubainika
*Teknolojia ya mawasiliano yafichua siri zao
MTANDAO wa watu wanaodhaniwa kuwa washirika wa karibu wa mtuhumiwa wa kupanga njama za kutekeleza ugaidi, Joseph Ludovick, umeanza kufichuka.
Taarifa za kufichuka kwa mtandao huo, zimekuja zikiwa zimepita siku tatu baada ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kutangaza orodha ya majina ya watu mbalimbali, wakiwemo viongozi wa serikali, kiliodai kuwa ndio wanaopanga mipango ya kishetani kisha kuwasingizia watu wengine.
Duru za habari kutoka vyanzo mbalimbali vya MTANZANIA Jumatano zimeeleza kuwa, taarifa za awali za kikachero zilizokusanywa katika mfumo wa mawasiliano ya simu ya kiganjani ya Ludovick zimeonyesha kuwa amekuwa na mawasiliano ya karibu na baadhi ya wanahabari waliopata kufanya kazi kwa karibu na Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri, Absalom Kibanda.
Mawasiliano hayo yanadaiwa kuwa ni ya mazungumzo ya simu na ya kumtumia fedha kupitia mitandao ya kifedha ya simu za kiganjani.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, mbali na wanahabari hao, pia uchunguzi umeonyesha kuwa Ludovick amekuwa na mawasiliano ya karibu na baadhi ya wanasiasa wa Chadema, viongozi wa juu serikalini na katika Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Mmoja wa makachero aliyezungumza na gazeti hili (jina lake tunalifahadhi) alieleza kuwa taarifa za uchunguzi wa awali uliofanywa kwenye mfumo wa mawasiliano ya simu ya Ludovick zimeonyesha kuwa mtuhumiwa huyo amekuwa akiwasiliana kwa karibu na wahariri waandamizi wawili, waandishi wa habari na wachangiaji wa makala katika magazeti mbalimbali nchini.
Kachero huyo aliwataja wahariri wanaodaiwa kuwa na mawasiliano ya karibu na mtuhumiwa Ludovick ambao ni Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Jamhuri, Deodatus Balile na Mhariri Mtendaji wa gazeti la Tanzania Daima, Ansbert Ngurumo.
Balile na Ngurumo, kwa nyakati tofauti wamepata kufanya kazi na Kibanda. Ngurumo na Kibanda walifanya kazi pamoja katika Kampuni ya Habari Corporation Ltd, wakiwa waandishi wa habari wa gazeti la kila wiki la Rai na baadaye walifanya kazi pamoja katika Kampuni ya Free Media Ltd, inayochapisha gazeti la Tanzania Daima, ambako Kibanda alikuwa Mhariri Mtendaji na Ngurumo akiwa Naibu Mhariri Mtendaji.
Kwa upande wake Balile, alipata kufanya kazi na Kibanda katika Kampuni ya Mwananchi Communication Ltd na muda mrefu baadaye Kibanda alichukua nafasi ya Balile ya Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya Free Media, baada ya kuondoka kwenda masomoni nchini Uingereza.
Taarifa za uchunguzi wa kikachero zilizonaswa na MTANZANIA Jumatano zimeeleza kuwa, Ngurumo, mara kadhaa, amepata kufanya mawasiliano ya mazungumzo na Ludovick kupitia simu yake ya kiganjani na pia alipata kumtumia fedha kupitia simu yake hiyo ya kiganjani.
Duru za uchunguzi zinaonyesha kuwa baada ya tukio la Kibanda siku sita baadaye, Ngurumo aliandika kupitia ukurasa wake wa facebook kuwa ameibiwa simu yake hiyo aliyokuwa akiitumia kufanya mawasiliano na Ludovick.
Katika ujumbe wake huo, Ngurumo aliandika kuwa; “Kuna mtu ameibia simu yangu yenye laini mbili - Tigo (0719001001) na Airtel (0782172665) - tangu juzi na anatumia namba hizo kutapeli pesa kwa watu ambao majina yao yamo kwenye contact list. Anawatumia watu meseji, hapigi wala hapokei simu anapopigiwa. Anadai kwamba mimi nina shida naomba msaada na anapendekeza kiwango cha pesa za kutumiwa.
“Wapo wachache ambao wameibiwa tayari na wengine walitaka kuthibitisha kama ni mimi, wakapiga simu hakupokea. Wanaojua namba zangu za simu wameniuliza kupitia simu yangu ya Voda, wakagundua ni mtego wa tapeli. Kwa taarifa hii, nawajulisha wote wanaonifahamu na wasionifahamu watakaoombwa pesa na mimi kutoka kwa yeyote, wasitoe kabisa. Anayeomba pesa hizo si mimi, ni tapeli!”
Ujumbe wake huo ulizua maswali kwa baadhi ya watu ambao walihoji ni kwa vipi matapeli hao waliweza kufahamu mpaka namba ya siri ya M-pesa au Tigo-pesa yake kiasi cha kufikia kupokea fedha kupitia namba zake hizo za simu?
Wengine walionyesha shaka, wakimuuliza ni kwa nini hakuwahi kwenye kampuni za hizo simu kwenda kuzifunga na badala yake akaziacha kuendelea kutumika?
Mmoja wa watu waliochangia katika ukurasa huo wa Facebook, France Rubian, aliandika akihoji; “Da..! Muda wote huo kaka kwa nini ukae kimya? Achilia mbali kuibiwa, mbona angeweza hata kukuharibia mambo mengine kama akiwa na nia hiyo? Hapa panazuka mjadala mreeeefu usiokuwa na majibu sahihi. Simu imeibiwa, wewe kwa muda wa siku2 hujachukua hatua, aliyeiba anaomba hela kupitia hizo namba zako, ‘password zako pia anazo ndiyo maana anaweza kuchukua hela.... Mh! Kazi kwelikweli.”
Tambo za kiuchunguzi zilizofanywa na gazeti hili, zimebaini kuwa moja ya namba hizo za Ngurumo, 0719 001 001 ambayo ndiyo imeandikwa kwenye safu ya bodi ya wahariri kupitia gazeti analoliongoza la Tanzania Daima, hadi jana ilikuwa inaonyesha kuwa imesajiliwa kwa jina la Subira Ramadhani.
Alipoulizwa Ngurumo kupitia simu yake ya kiganjani na MTANZANIA Jumatano kuhusu uhusiano wake na Ludovick na iwapo ana ushirika naye wowote wa kibiashara, alisema anamfahamu kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa, lakini hana ukaribu naye sana wala hashirikiani naye katika biashara yoyote.
Ngurumo alisema alimfahamu Ludovick akiwa katika harakati zake za kisiasa mkoani Kagera, baada ya kuunganishwa na Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chadema, Wilfred Lwakatare, aliyeeleza kuwa ni msaidizi wake wa kisiasa.
“Nilimfahamu kijana huyu nikiwa katika harakati zangu za kisiasa mkoani Kagera na nilifahamishwa kwake na Lwakatare, ni msaidizi wake. Alianza kunizoea taratibu na baadaye aliniomba kunisaidia kazi za blog yangu kwa madai kuwa hana kazi na alidai pia kuwa huwa anamsaidia Mjengwa kazi za blog yake, lakini kabla sijaanza naye kazi akawa amekamatwa,” alisema Ngurumo.
Alipoulizwa mazingira yaliyosababisha amtumie fedha kupitia simu yake ya kiganjani, Ngurumo alisema Ludovick alipata kumuomba fedha za kumsaidia kuhama mahali alipokuwa akiishi, lakini alishindwa kumsaidia kwa sababu hakuwa nazo na mara ya pili alimuomba Sh 50,000 baada ya kupata wageni ghafla nyumbani.
“Aliniambia mama mkwe wake amekuja na hana hela, akaniomba Sh 50,000, nikamwambia hizo nyingi sana, basi nikatafuta kiasi kidogo nikamtumia, sikumbuki nilimtumia Sh ngapi, lakini nadhani ni Sh 20,000 au 30,000.”
Aidha, taarifa zaidi zinaeleza kuwa Balile, ambaye aliteuliwa na Jukwaa la Wahariri kuwa mmoja wa wajumbe wa timu ya kuchunguza tukio la kuvamiwa na kuteswa kwa Kibanda, amekuwa akifika ofisini kwa Ngurumo na kufanya mazungumzo naye kwa muda mrefu.
Kwa upande wake Balile, naye alipoulizwa kupitia simu yake ya kiganjani kuhusu uhusiano wake na Ludovick, alisema alimfahamu kijana huyo kupitia mawasiliano ya mitandao ya kijamii ambapo alianza kujenga naye ukaribu kabla hawajaanza kuwasiliana kwa simu.
Balile alisema, Ludovick alimueleza kuwa anavutiwa na uandishi wake wa makala na aliomba amfundishe kazi ya uandishi wa habari, jambo ambalo hakuweza kulifanya kutokana na majukumu yake mengi.
Hata hivyo, alivyoulizwa iwapo amekuwa akimtumia fedha Ludovick, alisema hajawahi kumtumia hata mara moja, licha ya kumuomba mara kadhaa na kutaja mara ya mwisho aliyomuomba akiwa mkoani Iringa, kwa maelezo kuwa alikuwa amekwama nauli ya kwenda Makambako, hivyo aliomba kutumiwa Sh 20,000 kwa ahadi ya kuzirudisha baada ya kurejea Dar es Salaam.
Alieleza zaidi Balile kuwa, alitafuta kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya kumtumia, lakini kabla hajatuma alipata taarifa kuwa amekamatwa na polisi.
Alipoulizwa Balile iwapo amewahi kujadili mwenendo wa mwandishi yeyote wa habari na Ludovick na hata kumpatia mawasiliano yake, alikiri jambo na kueleza kwa ufupi kuwa ni kweli alipata kutoa mawasiliano ya namba za simu ya mmoja wa waandishi wa habari kwa Ludovick, lakini baada ya kupata habari za kukamatwa kwa mkanda wa Lwakatare, alishtuka na kuamua kujipeleka mwenyewe polisi kueleza namna alivyotoa namba hiyo kwa Ludovick na mambo mengine anayoyajua kuhusu Ludovick.
Vyanzo vingine vya habari vya MTANZANIA Jumatano vimeeleza kuwa miezi michache kabla ya Ludovick kutiwa nguvuni akituhumiwa kushiriki mipango ya kigaidi, alijaribu pasipo mafanikio kujenga uhusiano wa karibu na Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Mwananchi, Dennis Msaki.
Vyanzo hivyo vya habari vinamtaja Balile kufanya kazi ya kuwaunganisha Ludovick na Msaki, vikidai kuwa ni Balile ndiye aliyempigia simu Msaki kumtaarifu kuwa Ludovick ni kijana wake na ana shida ambayo Msaki anaweza kuitatua, hivyo amempa namba yake ya simu ya kiganjani ili awasiliane naye.
Kwamba siku chache baada Msaki kupokea ujumbe wa Balile, alipigiwa simu na Ludovick ambaye kwanza alimpongeza kwa uandishi mzuri wa makala, kisha akamuomba awe mwalimu wake wa uandishi wa habari, jambo ambalo lilimshangaza Msaki, kwa sababu haandiki makala magazetini na hivyo alimueleza kuwa taarifa alizopatiwa siyo sahihi na kumkatia mawasiliano.
Mbali na Balile na Ngurumo, taarifa za kikachero zinaeleza zaidi kuwa wapo pia baadhi ya waandishi wa habari wanaotajwa kuwa na mawasiliano ya simu na Ludovick, jambo linalozua hofu kuwa Mtandao ambao aliutaja Mjumbe wa Baraza Kuu la Chadema, Mabere Marando ni mkubwa na si tu kwamba unaigusa serikali na CCM pekee, bali pia wanahabari na baadhi ya wanasiasa.
Jumapili Aprili 14, Marando, alijitokeza mbele ya waandishi wa habari na kutangaza orodha ya majina ya watu mbalimbali, wakiwemo viongozi wa chama na serikali kuwa ndio wahusika wa mipango ya kishetani.
Miongoni mwa viongozi wa juu wa CCM waliotajwa na Marando ni Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Mwigulu Nchemba, aliyedai kuwa uchunguzi wake ulibaini simu yake kufanya mawasiliano ya mara kwa mara kwa watuhumiwa wa ugaidi. Hata hivyo, Mwigulu amekwisha kaririwa akieleza kuwa yuko tayari kueleza kile anachokijua kuhusu mtandao wa ugaidi mbinguni na duniani.
Marando aliwaambia waandishi wa habari kuwa kutokana na uzoefu wa kazi yake ya ushushushu, amechunguza na kubaini kuwa watu hao aliowataja ndio wahusika na vitendo viovu na kuahidi kuwa ataongoza jopo la mawakili wa Chadema kumteteta Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa chama hicho, Wilfred Rwakatare, anayekabiliwa na tuhuma za kushiriki kupanga ugaidi mahakamani.
Tags
Check mambo
ReplyDelete