MSHAMBULIAJI wa Yanga, Jerry Tegete, huenda akaiwahi mechi ya mwisho ya Ligi Kuu Bara dhidi ya wapinzani wakubwa wa Jangwani, Simba, itakayochezwa Mei 18, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar.
Tegete ambaye aliuanza vizuri mzunguko wa pili wa ligi hiyo kwa kuonyesha uwezo mkubwa wa kufunga mabao, ameshindwa kuendelea na kasi yake hiyo kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya goti. Mpaka sasa ameshaifungia timu yake mabao saba ya ligi lakini katika mechi za hivi karibuni alishindwa kushiriki kutokana na maumivu hayo ya goti ambayo yanamtesa kwa muda mrefu sasa.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Daktari Mkuu wa Yanga, Nassoro Matuzya, alisema mshambuliaji huyo atalazimika kukaa nje ya uwanja kwa zaidi ya wiki mbili kabla ya kurejea uwanjani kuanza mazoezi mepesi.
Hiyo inamaanisha kuwa Tegete anaweza kuwa fiti kuikabili Simba katika mchezo unaosubiriwa kwa hamu kubwa na wadau wengi wa soka nchini.
“Siwezi kusema kuwa Tegete ataiwahi mechi dhidi ya Simba, lakini kikubwa atakaa wiki mbili nje ya uwanja akiuguza majeraha hayo kabla ya kurejea uwanjani. “Wiki moja ataitumia kwa ajili ya matibabu na wiki nyingine moja kwa ajili ya kupumzika kabla ya kuanza mazoezi.”