Tukio la kutekwa Ludovick ladaiwa kuwa ni 'feki' Polisi washikwa kigugumizi
0
April 21, 2013
*Tukio la kutekwa Ludovick ladaiwa kuwa ni 'feki'
*RB yake yazua utata, Polisi washikwa kigugumizi
JIMEIBUKA hofu ya kuwepo mpango mahususi unaoratibiwa na Serikali kufichua njama za kigaidi, ambazo zinadaiwa kutekelezwa na baadhi ya viongozi wa kisiasa wanaoheshimika katika jamii, MTANZANIA Jumapili limebaini.Taarifa za uhakika zilizolifikia gazeti hili zinaeleza kuwa, kukamatwa kwa mtuhumiwa namba mbili katika kesi ya ugaidi iliyofunguliwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Ludovick Joseph, ni utekelezaji wa mpango huo.
Imedaiwa kuwa, kuna utata mkubwa wa usahihi wa taarifa za tukio la Ludovick kutekwa na watu ambao hawajafahamika hadi sasa na hata taarifa za kutekwa kwake alizodai kuzifikisha katika kituo kidogo cha polisi Kigogo, nazo zina utata.
Kwa mujibu wa wapasha habari wetu, taarifa za kutekwa kwa Ludovick na kunyang’anywa vitu vyake vyote alivyokuwa navyo, zikiwemo nguo alizokuwa amevaa na hata madai kuwa aliripoti tukio hilo katika kituo cha Polisi Kigogo siyo za kweli, bali zimetengenezwa ili kufanikisha mpango huo.
Ludovick alidai kutekwa usiku wa Jumanne ya Machi 5, mwaka huu, akiwa eneo la Sinza ambako alisema alitoa taarifa zake katika Kituo cha Polisi cha Kigogo na kufunguliwa RB yenye namba KIG/RB/318/2013.
Taarifa ya kutekwa kwake aliiandika mtandaoni na ilisomeka hivi; ‘Leo usiku, yapata saa tano na nusu, niliachana na Maggid Mjengwa maeneo ya Shekilango tukitokea Rose Garden. Yeye alielekea hotelini alikofikia sehemu fulani Kariakoo nami nikasubiri kigari kuelekea nyumbani kwangu.
Hapo Shekilango, magari yalichelewa kidogo, pembeni ilipaki bajaji ikiwa na watu wawili na dereva ndipo wakaniambia twende tuchangie mia tano tu kwenda Ubungo Mataa, nikakaa katikati ya hao jamaa.
Ghafla wakakata kona na kuanza kuelekea Mabibo huku wakiulizana kama wako kamili na mwingine kujibu yuko kamili. Nikajua tayari niko mikononi mwa majambazi na sikujua wako kamili namna gani, kwa hiyo nikaamua kuwa mtulivu.
Tulipofika relini karibu na Mabibo wakanipokonya begi lakini, hawakulifungua. Ndani yake kulikuwa na laptop, toshiba kubwa na chaji yake, kamera ndogo ya digital na USB yake, modem ya zantel na card reader. Tulipofika maeneo ya Loyola Sekondari, nikawasihi wanishushe ili nirudi mwenyewe, wakaniambia safari ile inaishia Jangwani.
Nikaingiwa na wasiwasi mkubwa na nia yao hasa, maana wameshanipokonya begi kwa nini wasiniachie? Lakini niliendelea kuwa mtulivu ili kutowaprovoke.
Tulipovuka Kigogo mwisho kwenye giza karibu na msikiti, wakasimama pembeni ya barabara na kuniamuru kushuka, nikashuka na kuanza kuwadai begi langu, ndipo mmoja akasema wamekuwa wastaarabu mimi naanza kuwadharau. Ghafla akanivuta kwa nguvu kunirudisha kwenye kibajaji akamwambia mwenzie wanisachi kama nina vitu vingine, wakanisachi na kuchukua pesa, nilikuwa na elfu 35 na simu mbili ndogo za nokia moja yenye line mbili.
Kisha mmoja akatoa ‘order’ nivuliwe nguo. Nikavuliwa viatu, T-shirt na suruali nikabaki na nguo za ndani pekee. Wakanishusha na kuniacha hapo.
Kurudi nyuma kama hatua kumi tu ndipo kituo kidogo cha polisi Kigogo nikaanza kutoa maelezo hapo kwa zaidi kama ya saa mbili nikiwa uchi na nguo za ndani tu. Nikiwa hapo nikasikia polisi wakiwasiliana juu ya tukio la kupigwa vibaya Absalom Kibanda, kwenye redio calls.
Ilikuwa yapata saa nane, baada ya kuchukuliwa maelezo polisi walinipatia gari nikaelekea hotelini kwa Maggid, ambaye saa kumi aliamshwa na kunichukulia chumba hapo nikapumzika. Ameniazima nguo zake ndizo nimevaa bado hadi sasa naelekea kituo cha Polisi Magomeni kwenda kupewa mpelelezi wa kesi yangu. Namba ya kesi yangu Kigogo ni KIG/RB/318/2013, wizi kutoka maungoni.’
Wakati Ludovick akiwa ametoa maelezo hayo kwa jamii kupitia mitandao ya kijamii, polisi wameshindwa kuthibitisha taarifa za kutekwa, kuporwa na kupokea taarifa yake aliyodai kuitoa kituo kidogo cha polisi Kigogo.
Polisi katika kituo kidogo cha Kigogo waliohojiwa na MTANZANIA Jumapili kuhusiana na taarifa za Ludovick, walionekana kurushiana mpira kuzizungumzia.
Askari aliyekutwa kituoni hapo alipoulizwa kuhusu taarifa hizo alisema taarifa za matukio mbalimbali hufunguliwa hapo, lakini huhamishiwa Kituo cha Polisi cha Magomeni kutokana na udogo wa kituo hicho, hivyo kumtaka Mwandishi kufuatilia suala hilo katika Kituo cha Polisi Magomeni.
Gazeti hili lilipofika Kituo cha Polisi Magomeni, kwa Askari Mpelelezi liliyeelekezwa kuwa anahusika na kesi ya Ludovick aliyetajwa kwa jina moja la Chuki hakuwepo bali lilipewa namba ya simu yake ya kiganjani na alipotafutwa, naye alikana kuhusika na suala hilo na kuelekeza atafutwe askari polisi aliyetajwa kwa jina la Lukwamba Sanga.
Alipopigiwa Sanga na kuulizwa kuhusu sakata hilo, kwanza alikiri kuwa yeye ndiye mpelelezi wa kesi hiyo na kueleza kuwa ni kweli Ludovick alifungua RB katika kituo cha Polisi cha Kigogo lakini hakuwa tayari kutoa namba ya RB hiyo.
Alieleza kuwa mwenye mamlaka ya kutoa namba hiyo ni Mkuu wa Upelelezi wa Kituo ambaye hata hivyo hakupatikana, lakini ofisa mwingine kituoni hapo alieleza kuwa namba hiyo inaweza kutolewa kwa idhini ya Kamanda wa Mkoa wa Polisi Kinondoni, Charles Kenyela.
Kamanda Kenyela alipotafutwa, alisema anahitaji muda kuipata namba hiyo, kwa sababu ana majukumu mengi hivyo atafutwe baadaye. Lakini alipotafutwa tena simu yake ya kiganjani ilikuwa haipatikani.
Hata alipopigiwa simu tena jana iliita mfululizo pasipo majibu.
Wachambuzi wa masuala ya saikolojia wanadai dalili zinaonyesha kuwapo kwa uwezekano wa Ludovick kushiriki tukio la kutekwa na kupigwa kwa Mhariri Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya New Habari (2006) Ltd, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri, Absalom Kibanda.
Wanasema ni kawaida kuwa watu wanaojihusha na matukio ya aina hii, baada ya kuyatekeleza huchanganyikiwa, hivyo hata kitendo cha Ludovick kukimbilia kuandika katika mtandao wa ‘facebook’ kuwa naye alitekwa kinaweza kuchukuliwa katika mtizamo huo.
Maswali ya kujiuliza
Ikiwa ni zaidi ya mwezi mmoja sasa baada ya kuvamiwa na kuteswa kwa Kibanda na siku chache baadaye kukamatwa kwa Ludovick akihusishwa na tuhuma za kupanga ugaidi, yapo maswali mengi miongoni mwa jamii ambayo hayajapata majibu kuhusu matukio hayo.
Swali kubwa linaloumiza vichwa vya wengi hivi sasa ni namna ambavyo Ludovick alifanikiwa kujipenyeza na kufanikiwa kujenga mtandao wa masiliano ya simu za mkononi na katika mitandao ya kijamii na Wahariri mbalimbali wa Vyombo vya Habari.
Tayari Wahariri wawili, Deodatus Balile na Ansbert Ngurumo, wamekwishatajwa kuwa na mawasiliano ya muda mrefu na Ludovick na kwamba kuna baadhi ya taarifa muhimu za waandishi na wahariri ambazo Ludovick alikuwa akizipata kupitia mawasilino yake hayo.
Kutajwa kwa wahariri hao kuwa washirika wa karibu kimawasiliano na Ludovick, kuliibua hisia kuwa Wahariri hao, waliingizwa katika mtandao wa Ludovick na kuanza kufanya kazi zake pasipo wao wenyewe kujua au wakiwa na ufahamu huo.
Lakini pia wadadisi wa mambo wamekuwa wakihoji nguo za Ludovick zilipo baada ya kile kinachodaiwa kuwa tukio hilo la kudai kutekwa ni feki.
Hali kadhalika hatua ya Ludovick baada ya kuachana na Mjegwa na kupanda bajaji iliyokuwa na watu wawili kisha akakaa katikati kwa nauli ya shilingi mia tano huku akiwa na pesa taslimu shilingi 35,000, begi lenye laptop toshiba kubwa, chaja yake, kamera ndogo ya digital na USB yake, modem ya zantel na card reader, jambo linaloonyesha kuwa alikuwa na uwezo wa kuchukua usafiri salama zaidi.
Aidha, mkanganyiko wa maelezo ya Ludovick na yale yaliyotolewa na Mjengwa ambako yeye (Ludovick) alidai kupewa gari na polisi kumpeleka hotelini kwa Maggid, huku Maggid akidai alifika hapo kwa usafiri wa teksi, nayo yanazidi kuacha swali gumu la kupata ukweli wa sakata hili zima.
Kuhusishwa kwake na tukio la Kibanda Siku na wakati ambao Kibanda alitekwa na kuteswa, Ludovick naye alidai kutekwa na majambazi akiwa eneo la Sinza, jirani na mahali ilipo ofisi ya Kibanda. Ludovick alidai kutekwa na watu wasiojulikana majira ya saa tano usiku siku ya Jumanne ya Machi 5, mwaka huu, ambapo watekaji wake walimnyang’anya vitu vyake mbalimbali na kumvua nguo zote pamoja na kuchukua simu zake mbili.
Ingawa katika uchunguzi wake gazeti hili liliambiwa kuwa simu yake iliendelea kutumika katika maeneo ya mnara wa Sinza karibu na ofisi anakofanyia kazi Kibanda siku mbili mara baada tukio la kuteswa kwa Mhariri huyo. Pamoja na hilo, siku mbili kabla Kibanda hajatekwa, anadaiwa kufanya mawasiliano na kiongozi mmoja mkubwa wa chama cha siasa.
Ahusishwa na video ya Lwakatare
Yuko mikononi mwa sheria na alishafikishwa Mahakamani pamoja na Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Wilfred Lwakatare, kutokana na mipango ya kudhuru watu, wakiwemo waandishi wa habari pamoja na suala la ugaidi.
Inaelezwa kuwa watu hao wamekuwa karibu kwa muda mrefu ambapo wote ni wenyeji wa Mkoa wa Kagera, na kwa mujibu wa watu wa karibu na mahusiano yao, walisema kuwa Ludovick amepata kumsaidia kufanya kampeni za kuwania ubunge wa Jimbo la Bukoba Mjini mwaka 2000.
Ludovick ni nani?
Ludovick, mbali na kuwa na ukaribu na Lwakatare, pia alikuwa mtu wa karibu na Mjengwa, akimsaidia katika shughuli za blog yake, pamoja na wahariri mbalimbali wa habari.
Ludovick pia wapo wanaomtambua kama mtu wa Idara ya Usalama wa Taifa.
Mjengwa pia aliwahi kukiri kutofahamu kazi halisi aliyokuwa akiifanya Ludovick mtaani, lakini katika maelezo yake aliyoandika kupitia kwenye mtandao wa Jamii Forum, Mjengwa alisema anamfahamu Ludovick tangu akiwa Chuo Kikuu (DUCE) na kwamba ni mmoja wa Watanzania wengi waliomfahamu kupitia kazi zake magazetini.
Tags