Wabunge wa CCM walikutana katika kikao cha dharura kilichoongozwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kujadili hatua ya Bunge kukataa bajeti hiyo kwa maelezo kwamba haina suluhisho la kuwaondolea wananchi matatizo ya maji.
Kelele za wabunge wa CCM na wale wa upinzani zilimlazimisha Spika wa Bunge, Anne Makinda kuiondoa bungeni na kuitaka Serikali ikajipange upya na kuiwasilisha Jumatatu.
Baada ya kuahirishwa kwa kikao cha Bunge jana mchana, wabunge wa CCM walikutana na habari kutoka ndani ya kikao hicho zinasema wabunge Kangi Lugola (Mwibara) na Deo Filikunjombe (Ludewa) walishambuliwa kutokana na kile kilichodaiwa kwamba wamekuwa wakiidhalilisha Serikali ya CCM bungeni.
Habari zinadai kwamba waliowashambulia wabunge hao ni wenzao, Saidi Nkumba (Sikonge) na Livingstone Lusinde (Mtera) ambao kwa nyakati tofauti walitamka kwamba hawaisaidii Serikali na kwamba bora wakahamia upinzani kuliko kuendelea kukichafua chama hicho.
“Kimsingi jamaa walibanwa sana walitaka Filikunjombe na Lugola wafukuzwe uanachama kwa sababu wanaishambulia sana CCM bungeni,” kilisema chanzo hicho.
Chanzo kingine kilisema kuwa wabunge hao walipata utetezi wa wabunge wawili, Beatrice Shellukindo (Kilindi) na Peter Serukamba (Kigoma Mjini) ambao walikaririwa wakisema kwa nyakati tofauti kwamba Lugola na Filikunjombe hawajakosea chochote kwani wanaeleza hali halisi ilivyo.
Baada ya mjadala huo, Pinda alikaririwa akimwelekeza Katibu wa Wabunge wa CCM, Janister Mhagama kumwandikia barua Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana kuhusu suala hilo ili liwe ajenda katika mkutano baina ya wabunge wa CCM na Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete ambao unatarajiwa kufanyika mwezi ujao.
Habari zinadai kuwa hoja ya kutupwa wa Bajeti ya Maji haikujadiliwa hata kidogo, kwani baada ya Pinda kuwaarifu wabunge kuhusu kilichotokea bungeni, wabunge hao wa CCM katika kikao hicho cha ndani walianza kumsaka mchawi kutoka miongoni mwao.
Akiiondoa bajeti hiyo jana mchana, Spika Makinda aliitaka Kamati ya Bunge ya Bajeti inayoongozwa na Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), Andrew Chenge pamoja na Wizara ya Fedha na Wizara ya Maji kukutana kuiangalia upya na kutafuta jinsi ya kupata fedha za kuongeza kisha iwasilishwe Jumatatu ijayo.
Hatua ya Makinda ilikuja baada ya mashambulizi makali ya kuikataa hivyo kusema haoni sababu za hoja hiyo kuendelea kujadiliwa, kwani tayari ilikuwa imelalamikiwa na wabunge wengi kutoka pande zote.
“Mapema leo Mheshimiwa Mwigulu Nchemba aliomba mwongozo wangu, lakini na mimi nasema toka jana hadi leo hii naona hoja za wabunge kuhusu jambo hili hakuna anayeunga mkono,” alisema Makinda na kuongeza:
“Pamoja na shutuma nyingi kuhusu Kamati ya Bajeti niliyounda na kumteua Mheshimiwa (Andrew) Chenge kuwa mwenyekiti, sasa naagiza kamati hiyo ikutane na Wizara na Serikali ili watafute jinsi ya kupunguza tatizo hili na walete majibu hapa siku ya Jumatatu, hivyo naahirisha shughuli za Bunge hadi Jumatatu asubuhi.”
Makinda alilalamikiwa kwamba aliunda kamati hiyo kinyume cha kanuni za Bunge lakini jana alisema alifanya hivyo kwa kutumia Kifungu cha 5 cha Kanuni za Bunge ambazo zinampa mamlaka ya kufanya hivyo.