Bomu Arusha - Vatican yawasilisha taarifa UN

Tukio la kutupwa bomu katika Kanisa Katoliki la Joseph Mfanyakazi, Arusha limetua katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UN) baada ya kuwasilishwa na Balozi wa Vatican UN, Askofu Mkuu Frances Chullikatt. Askofu Chullikatt anakuwa kiongozi wa kwanza wa Vatican kutoa tamko kuhusiana na shambulizi hilo ambalo mmoja wa viongozi wake alikuwapo.

Bomu hilo lilirushwa katika kanisa hilo wakati likizinduliwa na Balozi wa Vatican nchini, Askofu Mkuu Francisco Padilla Mei 5, mwaka huu na kusababisha vifo vya watu watatu na kujeruhi zaidi ya 50. Wakati wa shambulizi hilo, Askofu Padilla na Askofu Mkuu wa Jimbo la Arusha, Josephat Lebulu walionusurika.

Akihutubia Kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, New York, Marekani juzi, Askofu Chullikatt alisema tukio lililotokea Arusha linadhihirisha kuwa kuna umuhimu ya kupambana na ugaidi katika Afrika ili kuimarisha amani na usalama wa kimataifa.“Unahitajika mshikamano na ushirikiano wa pamoja wa mataifa mbalimbali katika kuchukua hatua za maisha na kulinda haki za binadamu,” alisema Askofu Chullikatt, ambaye amekuwa mwakilishi wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa tangu mwaka 2010.

Askofu Chullikatt, ambaye ni mzaliwa wa India, alisema suala la ugaidi linahitaji kuzuiwa duniani kote na hasa Afrika kutokana na matukio hayo kuharibu maisha ya binadamu na kutokea katika maeneo wanayofanyia ibada. Askofu Chullikatt alisema pale ugaidi unapofanyika kwa kutumia dini, waumini na viongozi wao ni lazima wahakikishe wanapambana nao ili kuutokomeza.

Alisema suala la ugaidi linahitaji viongozi wa kisiasa, kijamii na kidini kulilaani kwani ni la kikatili katika maisha ya binadamu hivyo si vyema kukaa kimya suala hilo linapotokea. Askofu Chullikatt alisema ugaidi unaotokea Afrika unatakiwa kuangaliwa kimataifa ili kuzipa uwezo nchi hizo kupambana na kuzuia matukio hayo.

Shambulio la bomu dhidi ya kanisa la Arusha lilikuwa tukio la pili la ugaidi uliolenga kushambulia wageni nchini. Mara ya kwanza ilitokea mwaka 1998, wakati Ubalozi wa Marekani nchini ulipolipuliwa kwa bomu na kusababisha vifo vya watu kumi na moja huku 85 wakijeruhiwa.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad