Dar es Salaam. Uchaguzi Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania(TFF)
utafanyika Septemba 29 mwaka huu, ikiwa ni kutekeleza agizo la
Shirikisho la Soka la Dunia (Fifa).
Uamuzi wa kufanya uchaguzi huo Septemba 29
ulifikiwa Dar es Salaam jana baada ya kikao cha dharura cha Kamati ya
Utendaji ya TFF chini ya Leodegar Tenga.
Awali uchaguzi huo ulipangwa kufanyika Februali 24
mwaka huu, lakini Fifa iliufuta na kuagiza mchakato uanze upya baada ya
kubaini kuwapo na kasoro kadhaa.
Mbali ya kuagiza mchakato uanze upya, Fifa pia iliiamuru TFF iunde kamati ya maadili ya ngazi ya mwanzo wa uchaguzi na rufaa.
Akizungumza mara baada ya kikao hicho, Tenga
alisema kuwa, kamati ya utendaji imepokea maagizo ya Fifa na imekubali
kuyatekeleza bila kipingamizi.
“Tumepokea maagizo ya Fifa yanayotuelekeza cha kufanya, siyo TFF wala mtu mwingine yeyote anayeweza kuongeza jambo lingine.
“Tunatakiwa kuunda Kamati ya Maadili, Kamati ya
Rufani ya Maadili, kufanya marekebisho ya Katiba, mchakato mpya wa
uchaguzi, waliokuwapo na wapya waruhusiwe. Tumejitahidi kuhakikisha
uchaguzi uwe kabla ya Oktoba 30 mwaka huu kama Fifa walivyotuagiza,”
alisema Rais Tenga.
Tenga alisema notisi ya mkutano mkuu wa dharura
itatolewa Juni 12 au 13, wakati Juni 15 Kamati ya Utendaji ya TFF
itakutana kwa ajili ya kupokea mapendekezo kabla ya kuyapeleka tena
Fifa.
Kamati itakutana Julai 14 na 15 na kuunda Kamati ya Maadili na Kamati ya Rufani ya Maadili.