Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC-CCM) na Mstahiki Meya wa
Manispaa ya Ilala Jerry Silaa amewataka viongozi wa Chama cha Mapinduzi
kuwa na utaratibu wa kukosoana pindi wanapokosea badala ya kusubiri
vyama vingine viwasemee.
Hayo ameyasema wakati akikabidhi kadi za uanachama kwa Tawi jipya la
Chuo Kikuu cha Ushirika na Biashara (MUCCOBS) mkoani Kilimanjaro.
Silaa amesema kumekuwa na tabia ya viongozi wa CCM kuonea aibu hata
makosa yanapotendeka kwa viongozi wa ngazi za chama kwa kuogopa
kufukuzwa uanachama.
Pia amesema kukosoana ni sehemu ya kuleta maendeleo katika jamii yoyote ambayo inajali demokrasia ya kweli
Mjumbe huyo wa NEC taifa amesema vyama vya upinzani nchini vimepata
nguvu kubwa kutokana na baadhi ya watendaji wa CCM ngazi za vijiji,
kata, wilaya na mikoa kushindwa kuwawajibisha viongozi wanapokosea kwa
kuogopa kufukuzwa ama kutendea kitu chochote kibaya
Aidha Silaa alisema kitendo hicho kimewapunguzia heshima mbele ya
wananchi walioamini kuwa wanzilishi wa demokrasia nchini kupitia kupiga
kura hata kusababisha majimbo mengine kuchukuliwa na wapinzani.
Hata hivyo, Jerry Silaa katika kutoa kwake rai hiyo amewataka viongozi
hao kukosoana kwa utaratibu na kwamba anayekosea aangaliwe kama yeye na
sio kama chama kwani sio wote ni wachafu.
Kwa upande wake, Katibu wa CCM mkoa wa Kilimanjaro Steven Kazidi amesema
kutokana na kutokosoana baadhi ya wanasiasa wametumia mwanya huo huo
kuanzisha migomo katika vyuo vikuu hapa nchini kwa kudai kuwa CCM
iliyoko madarakani ndio imeyaleta hayo.
Kazidi ameongeza kusema wanansiasa hao wameendelea kumwaga sumu yao kwa
wanavyuo hao kuwa wataendelea kupata taabu endapo wataendelea kuichagua
CCM
Pia Katibu huyo maarufu kwa jina la “OFFSIDE” amewataka wanavyuo hao
kuzingatia elimu hadi watakapomaliza masomo yao na hatimaye wachague
chama cha siasa ambacho kitawaletea maendeleo
Kazidi amehitimisha kwa kusema migomo na maandamano yanayofanywa na
wavyuo kutokana na uchochezi wa kisiasa yamesababisha kuharibu
miundombinu ya vyuo husika zikiwemo samani na majengo
Awali akisoma taarifa ya Wanavyuo wa MUCCOBS kwa niaba ya wanachama wa
CCM mbele ya Mgeni Rasmi Jerry Silaa, David Waryoba amesema umefika
wakati kwa Chama cha Mapinduzi kufanya maamuzi dhidi ya wanaokichafua
chama kwa kutumia maslahi ya chama kufanya hujuma kwa wananchi kwa
manufaa yao kwa kupora rasilimali za taifa.
Hatimaye Mgeni rasmi alihitimisha kwa kuwakabidhi kadi wanachama wapya 155 kutoka MUCCOBS.
Habari kwa hisani ya Wavuti.