Akizungumzia kuhusu kutua kwa Kibadeni katika
klabu ya Simba, Kaimu Makamu wa klabu hiyo, Joseph Itang’ale alisema
mkataba rasmi bado hawajasaini na Kibadeni ila wanatarajia kumpa mkataba
wa miaka miwili au wa mwaka mmoja.
Kuhusu wana malengo gani na Kibadeni, Makamu huyo
alisema Kibadeni ndiye kocha pekee ambaye ameshawapa ubingwa Simba mara
tatu na alijenga timu ya vijana ya Simba ambayo mpaka sasa inafanya
vizuri.
Akizungumzia kwa nini wameamua kuachana na kocha
Patrick Liewig raia wa Ufaransa, Makamu huyo wa Simba alisema kocha
Liewig alikuwa akibagua watu ndani ya klabu ya Simba na kujiona yeye
ndiye yeye jambo ambalo lilikuwa likiwakera wachezaji, pia hajafanya
kazi yake vizuri katika kukinoa kikosi cha Simba.
Itang’ale alisema Simba wataanza mazoezi yao kesho
kwenye uwanja wa Kinesi, Dar es Salaam kwa ajili ya kujiandaa na
mashindano ya Kagame, ambapo kikosi chao kitakuwa chini ya Kibadeni.
‘’Tumemkabidhi mikoba yote Kibadeni na
tumekubaliana naye kila kitu na kesho ‘leo’ kocha huyo atakutana na
kamati zote za ufundi kwa ajili ya kueleza programu nzima tayari kwa
kuanza kazi,’’ alisema Itang’ale.
Pia Itang’ale alisema kuwa tayari wamemalizana na
kocha Liewig kwa amani na sasa wameamua kujenga Simba mpya kwa ajili ya
mashindano mbalimbali yaliyopo mbele yao.
Hata hivyo, kocha Kibadeni alipotafutwa na gazeti
hili kuzungumzia kutua klabu ya Simba alisema kuwa msimamo wake kama
ataendelea kuwa na Kagera Sugar au atajiunga na Simba utajulikana wiki
ijayo ambapo atatoa msimamo wake.