Rais Kikwete alikutana na wachezaji wa Stars aliowaandalia chakula cha mchana, jana Ikulu Dar es Salaam.
Kikwete alisema amefurahishwa na matokeo mazuri ya Stars, inayoshika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Kundi C, na kwamba sasa Watanzania wanaipenda baada ya kufanya vizuri kwenye mechi zilizotangulia.
“Kuna wakati hamasa ilipotea na kuwafanya baadhi ya mashabiki kuingia uwanjani wakiwa wamebeba mabango ya Best Loosers, huku yakiwa na maneno ya kejeli. Wengine waliacha kwenda na baadhi kushangilia hata timu pinzani,” alisema Kikwete.
“Kuna kipindi nilikuwa nafikiria hata kuacha kumlipa kocha wa timu ya Taifa na kuliacha jukumu hilo kwa TFF, hata hivyo niliona kocha atakufa njaa na kuendelea na uamuzi wa awali. Nafurahi kuona sasa kuna mafanikio makubwa, lakini tunatakiwa kuhakikisha tunafuzu kwa ‘kuzinyoa’ timu zote katika mzunguko huu wa pili,” aliongeza.
Alifafanua kuwa siku ambayo Tanzania ilifungwa na Msumbiji kwenye uwanja mkuu alipatwa na wakati mgumu kujibu swali la Rais Kagame wa Rwanda ambaye alitaka kujua matokeo ya mechi hiyo.
“Kufungwa kunatonyong’onyesha hata sisi ambao tunafuatilia michezo, hakikisheni mnatupa raha na mimi niko tayari kusaidia kila kitu,” alisema Kikwete huku akiipongeza kamati ya Opereshi Ushindi kwa kazi kubwa ya kuwapa hamasa wachezaji hao kwa kuwapa Sh30 milioni.
Awali, kaimu Mwenyekiti wa Operesheni Ushindi, Ramadhan Dau ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa NSSF, alisema kuwa jukumu lao kubwa ni kuhakikisha wanaondoa kero zote kwa wachezaji na maofisa wa timu hiyo ili waweze kucheza mpira katika mazingira mazuri.
Nahodha wa timu ya Taifa, Juma Kaseja alimshukuru Kikwete kwa mchango wake na kuahidi kufanya vyema katika mechi zote na kufuzu.
Kocha wa timu hiyo, Kim Poulsen naye alisema kuwa ingawa wanakabiliwa na kazi kubwa, wana uhakika kuwa watafuzu katika mashindano hayo ya Kombe la Dunia, CHAN na Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON).