Mashabiki pekee watainusuru Simba Mei 18

Kocha wa Azam FC, Stewart Hall ameipa Yanga nafasi kubwa ya kuibuka mbabe Mei 18, huku akibainisha silaha pekee ya Simba ni mashabiki wake watakaohudhuria pambano hilo.

Pambano hilo baina ya wapinzani hao wa jadi katika soka la Tanzania litakalopigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, ni kati ya mapambano mengine sita.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Hall alisema kuwa,Yanga ina nafasi kubwa ya kuibuka kidedea katika pambano baina yake na Simba kutokana na kikosi chenye wachezaji wenye uzoefu na wenye vipaji tofauti na Simba aliyodai wachezaji wake wanahitaji muda zaidi wa kupikwa.

“Kimsingi Yanga ina nafasi kubwa ya kuimaliza Simba, ina wachezaji wenye uzoefu wa kutosha, lakini si hivyo tu pia wana uwezo.

“Nadhani matokeo mazuri kwa upande wa Simba yatategemea sana uungwaji mkono kutoka kwa mashabiki wake ambao kwa siku za hivi karibu nimeona wako pamoja na wachezaji wao tofauti na awali,”alisema Hall.

Nao makocha wa timu hizo wakizungumza kutoka kwenye kambi zao visiwani Zanzibar, Patrick Liewig wa Simba na Ernie Brandts wa Yanga kila mmoja ametupa karata kwa kikosi chake kwamba kitamsambaratisha mwenzake.

“Wachezaji wangu wapo timamu kiakili na kimwili na wana morali ya hali ya juu ya kuhakikisha tunashinda mchezo dhidi ya wapinzani wetu Simba Mei 18,”.alisema Brandts.

Kwa upande wake, Liewig alisema kuwa, hapingi kwamba Yanga si timu bora kwenye ligi kuu msimu huu kwa vile kitendo cha kutwaa ubingwa.
“Tunajua kwamba Yanga ni mabingwa na tunalikubali hilo, lakini Simba nayo ni timu nzuri na ina mipango yake na mmojawapo ni kuhakikisha tunashinda mechi dhidi ya Yanga,”alisema Liewig.

Meneja wa timu ya Simba, Mganda Mosses Basena alisema jana kuwa timu yake itafanya mazoezi asubuhi na jioni kwenye Uwanja wa Mao Tse Tung na inatarajiwa kuondoka hapa kwenda Dar es Salaam Ijumaa.

Kocha wa makipa wa timu hiyo, James Kisaka alimsifu Liewig kuwa ni kocha nzuri kwani anaweka mbele nidhamu na kwamba sasa wachezaji wanamwelewa na kwa hiyo kikosi chao kitatisha.“Hawa mnawaita watoto, lakini si watoto. Uwezo wao ni mkubwa watawashangaza Jumamosi,” alisema.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad