Nditi ambaye alizaliwa Zanzibar mwaka 1994 kabla ya kujiunga na timu ya
Chelsea U13 miaka kadhaa iliyopita baada ya kuhamia England na familia
yake, katika siku za hivi karibuni ameibuka kuwa mjadala mkubwa suala
lake la kuichezea timu ya taifa ya Tanzania.
Siku za nyuma shirikisho la soka nchini TFF liliwahi kutoa ripoti
kwamba walijaribu bila mafanikio kuweza kumpata Adam kupitia ubalozi wa
Tanzania nchini Uingereza lakini hawakufanikiwa – ingawa Adam Nditi
mwenyewe anakanusha hakuwahi kupokea taarifa yoyote kutoka kwa TFF wala
ubalozi wa Tanzania UK kuhusu suala la kuja kuichezea Tanzania.
Kwa upande wa baba yake ya Nditi, aitwaye Eric Nditi amesema yeye
kama mzazi wa mchezaji huyo hayupo tayari kumruhusu mtoto wake kuja
kuitumikia Taifa stars mpaka pale taratibu zote zitakapofuatwa.
“Kiukweli kabisa kama taratibu zote hazitofuatwa Adam hatokwenda
Tanzania kuichezea timu ya taifa. Sitokubali mwanangu aende Tanzania kwa
taarifa za magazetini, kiutaratibu ili mchezaji aitwe kwenye timu taifa
inabidi benchi la ufundi la timu husika lijilidhishe na kiwango cha
mchezaji na sio kumuita tu bila kumfanyia scouting, pia inabidi mchezaji
atumiwe taarifa rasmi,” anasema Nditi.
Pia Eric Nditi amesikitishwa sana na taarifa kwamba mwanae hataki
kuichezea timu ya taifa ya Tanzania. “Tatizo la nchi yetu siasa zipo
kila mahala, bora wewe Shaffih umekuja mpaka huku kujua ukweli. Adam ni
mtanzania wa kuzaliwa na kukulia kwenye nchi hiyo na yupo tayari
kuichezea nchi yake ikiwa atatakiwa na mwalimu. Napenda kuona anaisadia
nchi yake lakini kwa utaratibu unaoeleweka.”