Dodoma/Arusha. Wakati maofisa wa Shirika la Upelelezi wa Marekani (FBI)
wametua Arusha, raia wanne wa Saudi Arabia na Watanzania wawili
wamekamatwa kwa tuhuma za kuhusika kulipua bomu lililoua watu wawili na
kujeruhi wengine 61 wakati wa ufunguzi wa Kanisa la Mtakatifu Joseph
Parokia ya Olasiti.
Waliofariki dunia ni Regina Longino Kurusei (45), mkazi wa Olasiti na
James Gabriel (16), ambaye alifariki usiku wa kuamkia jana.
Tukio hilo lilitokea wakati Balozi wa Vatican na Mwakilishi wa Papa
nchini, Francisco Montecillo Padilla alipokuwa akizindua kanisa hilo.
Akitoa maelezo kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda jana, Mkuu wa Mkoa wa
Arusha, Magesa Mulongo alisema raia hao wa Saudi Arabia walikamatwa jana
asubuhi baada ya tukio wakiwa kwenye gari wakielekea Kenya kupitia
Namanga.
Mulongo alisema raia hao wa kigeni waliingia nchini Jumamosi iliyopita
na siku iliyofuata ndipo kukatokea ulipuaji huo. Alisema lengo la
shambulizi hilo lilikuwa kumdhuru Askofu Padilla.
“Mtu ambaye tulimkamata jana (juzi Jumapili) ndiye aliyesaidia kuwapata
watu hawa wa Saudi Arabia na Watanzania hao,” alisema Mulongo.
Mulongo alisema maofisa wa FBI walifika jana saa tano asubuhi ili
kusaidiana na Polisi na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), katika
uchunguzi wa tukio hilo.
Maofisa hao wa FBI walikuwa Zanzibar ambako walikuwa wanachunguza kifo
cha Padri Evaristus Mushi ambaye aliuawa Februari 17, mwaka huu.
Hii itakuwa mara ya pili kwa wageni kuhusishwa na matukio ya ugaidi
nchini baada ya mwaka 1998 wakati raia kadhaa wa Misri wakiongozwa Fazul
Abdulla waliposhirikiana na Watanzania kadhaa akiwamo Ahmed Ghailani
kulipua ubalozi wa Marekani nchini na ule wa Kenya. Ghailani anatumikia
kifungo cha maisha nchini Marekani wakati Fazul aliuawa Somalia mwaka
2011.
Tamko la Serikali
Akitoa tamko la Serikali bungeni jana, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,
Dk Emmanuel Nchimbi alimtaja mmoja wa watuhumiwa wanaoshikiliwa
kuhusika na tukio hilo kuwa ni Victor Calisti Ambrose (20), mkazi wa Kwa
Mrombo Arusha ambaye ni dereva wa bodaboda. Alisema kijana huyo ndiye
anayetuhumiwa kurusha bomu hilo.
Waziri Nchimbi alitoa onyo kali kwa wanasiasa wanaopandikiza chuki za
kidini miongoni mwa Watanzania na kuishutumu Serikali kutokana na
matukio kama hayo. “Kuna wanasiasa ambao wanaona masilahi yao ni muhimu
kuliko maisha ya Watanzania, masilahi yao ni muhimu kuliko utulivu wa
Watanzania na masilahi yao ni muhimu kuliko umoja wa Watanzania.”
JK akatiza ziara, Bilal atoa ahadi
Rais Jakaya Kikwete, amekatiza ziara yake ya kiserikali nchini Kuwait
ili kurejea nyumbani kutokana na shambulio la bomu kwenye kanisa hilo.
Taarifa ya Ikulu imesema jana kwamba Rais Kikwete amelazimika kukatiza
ziara hiyo na kurejea nyumbani mara moja ili kuwa karibu na wafiwa
pamoja na wale waliojeruhiwa katika shambulio hilo la kigaidi.
Makamu wa Rais, Dk Gharib Bilal ameahidi kuwa Serikali itahakikisha wote
waliohusika na tukio hilo wanakamatwa na kufikishwa katika vyombo vya
dola.
Balozi wa Papa atoa tamko
Askofu Padilla ambaye jana alitembelea majeruhi katika Hospitali ya
Mkoa, Mount Meru, alieleza kustushwa na tukio hilo na kusema hakutarajia
kitu kama hicho kutokea wakati wa shughuli hiyo wakati Watanzania
wakijulikana ni watu wa amani.
Alilaani tukio hilo na kuvitaka vyombo vya usalama kufanya uchunguzi ili kubaini ukweli.
Kanisa Katoliki Arusha
Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Arusha jana liliitaka Serikali iwataje
waliohusika na tukio hilo la kigaidi huku likiwataka waumini wake
kutolipiza kisasi.
“Msimamo wa kanisa katika hili, ni kuwataka waumini wasilipize kisasi
kama ambavyo alisema Yesu Kristo kuwa msilipize kisasi, muwe tayari
kushinda ubaya kwa wema,” alisema Askofu Josephat Lebulu na kuongeza:
EU
Jumuiya ya Umoja wa Ulaya (EU), imetaka kuharakishwa kwa uchunguzi wa
tukio hilo na kuonya kuwa matukio kama hayo yanaweza kulitumbukiza taifa
kwenye machafuko.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Balozi wa Umoja
huo nchini, Filiberto Ceriani-Sebregondi alisema Tanzania inapaswa
kufahamu kwamba pasipo kujenga, kuendeleza na kusisitiza utamaduni wa
kuvumiliana, hali inaweza kuwa mbaya zaidi kwa siku za usoni.
Mlipuko Arusha: Watu 8 wakamatwa, wamo raia wanne wa Saudi Arabia
2
May 07, 2013
Tags
Mange kimambi
ReplyDeleteFBI walikuja kwa case ya hapa zenji kuuawa padre na wakamkamata muhusika fasta lkn cha kusikitisha eti mtuhumiwa hana case ya kujibu. Sasa mmewaleta Wa nn tena au kuwasumbua tu? Hata wakikamatwa watuhumiwa mahakama siitatuambia hawana case ya kujibu km huyu mzenji? Mnakera sana.
ReplyDelete