Ubabe ubabe tu. Usemi huu unaweza kutumika leo wakati miamba ya soka Tanzania, Simba na Yanga itakaposhuka dimbani kuumana katika pambano la kuhitimisha Ligi Kuu litakalopigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Mchezo baina ya mahasimu hao una sura tatu tofauti, kwanza kila timu inahitaji kuvuna pointi tatu ili kulinda heshima yake, kulipa kisasi na kuendeleza rekodi.
Yanga inasaka ushindi ili kunogesha ubingwa wake wa Ligi Kuu msimu huu, pia kulipa kipigo cha mabao 5-0 ilichokipata kutoka kwa Simba katika mechi ya Ligi Kuu iliyopigwa kwenye uwanja huo Mei 5, 2012.
Nao Wekundu wa Msimbazi, baada ya kupokonywa taji na kuambulia nafasi ya tatu, sasa wana kiu ya kutaka kuboresha rekodi yao ya kumtundika mpinzani wake Yanga mabao mengi zaidi katika mechi mmoja.
Kocha wa Yanga, Ernie Brandts akizungumzia matarajio yake kuelekea mtanange huo alisema:
“Bila kuifunga Simba ubingwa hauwezi kunoga, ndiyo maana tumejidhatiti kuhakikisha tunapata matokeo mazuri Jumamosi.”
Kwa upande wake Liewig alisema: “Tunajua Yanga ni Bingwa, lakini sisi pia tuna mipango yetu kama Simba ambayo ni kuhakikisha tunashinda mchezo wa mwisho na hilo nina uhakika litafanikiwa.”
Ubora wa vikosi:
Yanga itaingia uwanjani ikijivunia kikosi chenye wachezaji wazoefu katika mechi za ligi, lakini Simba itawategemea chipukizi wake walioitakatisha vyema mzunguko wa pili wa ligi Kuu, hususan Haruna Chanongo na Rashid Ismail.
Kiungo Mnyarwanda, Haruna Niyonzima atakuwa ‘mpishi’ mkuu wa mabao ya Yanga kwenye kipute hicho, kama itakayokuwa kwa Amri Kiemba wa Simba ambaye kiwango chake cha juu msimu huu kimewaacha wengi midomo wazi.
Rekodi za jumla:
Yanga na Simba zimekutana mara 100 katika mechi mbalimbali za Ligi Kuu, kati ya hizo Yanga ilishinda mara 37, Simba mara 32, huku mara 31 zikitoka sare.
Zaidi ya hapo, Yanga imetwaa ubingwa wa Ligi Kuu mara 23 wakati Simba imefanikiwa kunyakua taji hilo mara 18.